May 22, 2022 10:48 UTC
  • Mvua nyingine kali zalikumba jimbo la KwaZulu-Natal Afrika Kusini na kusababisha hofu kubwa

Jimbo la KwaZulu-Natal la Afrika Kusini ambalo bado halijatoka kwenye athari mbaya za maafa ya mafuriko makubwa kuwahi kutokea nchini humo, limekumbwa tena na mvua nyingine kubwa na kukumbushia mafuriko hayo ya mwezi Aprili.

Mvua kubwa zinaendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo ya jimbo hilo tangu juzi Ijumaa huku taarifa zikisema kuwa baadhi ya miundombinu tayari imeharibiwa kabisa hasa katika eneo la eThekwini.

Maafisa wa KwaZulu-Natal wamewataka wakazi wa jimbo hilo kuchukua tahadhari na kutoa amri ya kuhama wale wote ambao wako kwenye sehemu zenye hatari ya kukumbwa na mafuriko.

Serikali ya jimbo la KwaZulu-Natal imesema leo Jumapili kwamba imeanza zoezi la kutoa huduma za kuhamisha watu kama sehemu ya juhudi za kuhakikisha kila mtu anakuwa salama kutokana na mvua hizo kali. 

Mafuriko ya mwezi Aprili yamesababisha maafa makubwa nchini Afrika Kusini

 

Maafisa hao wamesema pia kuwa, Jeshi la Taifa la Afrika Kusini nalo limepeleka wanajeshi kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kukabiliana na hatari yoyote inayoweza kusababishwa na mvua hizo iwapo zitapelekea kutokea mafuriko.

Tayari baadhi ya barabara zimefungwa huku serikali ya jimbo la KwaZulu-Natal ikiwakataza watu kusafiri na kuwahimiza waakhirishe safari zao zote walizokuwa wamepanga.

Itakumbukuwa kuwa mwezi uliopita wa Aprili jimbo hilo lilikumbwa na mafuriko makubwa na mabaya zaidi kuwahi kutokea katika historia ya Afrika Kusini. Zaidi ya watu 440 walifariki dunia. Mafuriko hayo yaliharibu kikamilifu barabara, madaraja na majengo ya jimbo hilo.