May 22, 2022 10:51 UTC
  • Rais wa Misri awataka wananchi wake wale majani ya miti

Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri amewataka wananchi wa nchi hiyo wale majani ya miti na kusema kuwa, hata Mtume Muhammad SAW alifikia kula majani ya miti kwenye Bonde la Abu Talib wakati alipokuwa amewekewa vikwazo na washirikina wa Makkah.

Televisheni ya al Alam imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, el Sisi amesema hayo katika sherehe za uzinduzi wa miradi ya mustakbali wa sekta ya kilimo ya Misri na kusema: "Mtume Muhammad SAW na masahaba wake walifungiwa kwenye Bonde la Abu Talib kwa muda wa miaka mitatu, lakini masahaba wake hawakumwendea Mtume na kumdai maji na chakula... na hali ilikuwa ngumu kiasi kwamba walifikia hadi kula majani ya mti... lakini sisi hatuko hivyo, sisi tuna nguvu zaidi."

Matamshi hayo yamewakasirisha wananchi wengi huku wengine wakiyadhihaki katika mitandao ya kijamii ndani na nje ya Misri. Hali ya kimaisha nchini Misri imekuwa ngumu kiasi kwamba hivi sasa rais wa nchi hiyo anawataka wananchi wazidi kuwa wavumilivu na iwapo itabidi kula majani ya miti, wawe tayari kufanya hivyo.

Baadhi ya wananchi wa Misri wanaishi kwenye umaskini mkubwa

 

Mmoja wa watumiaji wa mitandao ya kijamii anayeitwa Ahmad Masoud ameandika: "Lakini Mtume alikuwa hawanyimi Waislamu haki zao, alikuwa hashirikiani na Mayahudi dhidi ya Waislamu, alikuwa hawatesi na kuwateka nyara Waislamu na wala alikuwa hafanyi jinai kwa ajili ya kutwaa na kubakia madarakani..."  

Hayo ni kwa mujibu wa tovuti ya "Arabi 21" ambayo imemnukuu mchangiaji mwingine anayeitwa Muhammad Abdur Rahman akielezea kushangazwa sana na matamshi hayo ya el Sisi. Ameandika: "Masha'Allah! Yaani hivi sasa unajifananisha na Mtume? Mtume alikuwa pamoja na wananchi kwenye kuhimili vikwazo hivyo. Hakuwa kama wewe uliyejijengea kasri na ambaye saa yako ya bei rahisi zaidi ni ya Pound milioni mbili [sarafu ya Misri]...