May 22, 2022 10:51 UTC
  • Rais wa Tshisekedi wa DRC aendelea na ziara ya kikazi nchini Burundi

Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo anaendelea na ziara yake katika nchi jirani ya Burundi. Tshisekedi yuko nchini Burundi kwa ziara rasmi ya siku tatu.

Alipowasili nchini humo jana Jumamosi, Rais Tshisekedi alipokewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Albert Shigiro na jana hiyo hiyo jioni alionana ana kwa ana na mwenyeji wake, Rais Evariste Nayishimiye. Lengo la ziara hiyo ni kujadiliana viongozi wa nchi hizo mbili, masuala ya kisiasa, usalama, biashara na uchumi.

Amma tukija upande wa jeopolitiki yaani siasa za kijiografia za kikanda, Tshisekedi anamuona Ndayishimiye kuwa mshirika wake wa kiistratijia na kimkakati katikati ya Paul Kagame na Yoweri Museveni, majirani wawili wanaotazamana kwa mashaka licha ya kwamba hivi sasa uhusiano wao umekuwa mzuri. Umuhimu wa Rais wa Burundi kwa Tshisekedi umezidi kuwa mkubwa kutokana na rais huyo kuhakikisha anashiriki katika takriban kila mkutano unaozungumzia ukosefu wa usalama katika kanda hiyo.

 

Tshisekedi na Ndayishimiye pia wana hamu ya pamoja ya kukomesha makundi yenye silaha ikiwa ni pamoja na RED-Tabara, waasi wa Burundi wanaoendesha uasi wao ndani ya ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo 2015. Huku Rais Félix Tshisekedi akipambana na makundi yenye silaha yanayohatarisha usalama wa nchi jirani na Kongo, Ndayishimiye naye kwa upande wake anapambana na harakati zote zinazohatarisha usalama huko DRC.

Nchi mbili za DRC na Burundi ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC na zina kila sababu ya kuimarisha uhusiano baina yao. Ndio maana zimetiliana saini hati mbili za maelewano kuhusu kujenga njia ya reli ambayo itaiunganisha Bujumbura na Kindu kupitia Bukavu na Kamituga.