May 23, 2022 09:44 UTC
  • Kundi la waasi wa M23 lakishambulia kikosi cha MONUSCO DRC

Kundi la waasi wa M23 limefanya mashambulio dhidi ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa MONUSCO huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa amelilaumu kundi la M23 linaloendesha harakati zake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kushambulia walinda amani wa tume ya Umoja wa Mataifa katika eneo la mashariki mwa nchi lenye machafuko.

Taarifa ya Bintou Keita, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa inatolewa baada ya jeshi la DRC kuanzisha mashambulizi dhidi ya kundi la M23 Alkhamisi iliyopita.

Taarifa ya Keita imelaani shambulio la kundi hilo dhidi ya wanajeshi wa serikali na kikosi cha walinda amani wa MONUSCO.

Waasi wa M23 walilenga kwa makusudi walinda amani wa MONUSCO ambao walijibu kwa risasi, kulingana na mamlaka yao,” Keita amesema.

Waasi wa M23 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

 

Jeshi la DRC na wanajeshi wa Monusco walianzisha operesheni ya pamoja dhidi ya waasi wa M23, taarifa ya Keita imeongeza.

Wakazi wa mji wa Goma wamesema kuwa, ujumbe wa MONUSCO ulitumia helikopta katika operesheni hiyo dhidi ya waasi wa M23.

Taarifa ya M23 imesema wapiganaji wao walilazimisha wanajeshi wa serikali kurudi nyuma na walikimbilia kwenye kambi ya Monusco, na hivyo kuwalazimu walinda amani wa Umoja wa mataifa kuingilia kati.

Mwezi Machi mwaka huu helikopta ya Umoja wa Mataifa iliyokuwa na askari jeshi wa kulinda amani wanane ilitunguliwa ikiwa katika shughuli ya kutathmini harakati za raia huko Kivu Kusini.