May 24, 2022 01:19 UTC
  • Chama cha al Nahdha chapinga uamuzi wa rais wa Tunisian cha kutangaza bodi ya katiba mpya

Chama kikuu cha upinzani nchini Tunisia cha al Nahdha, kimepinga vikali uamuzi wa Rais Kais Saied wa kuunda kamati ya ushauri kwa ajili ya kutunga katiba mpya na kusema kwamba kinapingwa kushirikishwa kwenye uvunjaji huo wa katiba ya wananchi.

Siku ya Ijumaa, Rais Saied alimteua profesa wa sheria, Sadok Belaid kuongoza kamati ya ushauri ya kutunga katiba mpya. Kamati hiyo inatakiwa kukabidhi ripoti yake tarehe 20 mwezi ujao wa Juni. Chama cha al Nahdha kimekataa kushirikishwa kwenye kamati hiyo. Chama hicho cha Kiislamu pamoja na vyama vingine vimetangaza kujitoa kwenye mchakato huo ambao vimeuita ni uvunjaji wa wazi na mkubwa kabisa wa utawala wa katiba.

Marekebisho makubwa ya katiba ya mwakaa 2014 yalishirikisha pande zote nchini Tunisia kuanzia vyama vya siasa, asasi za kiraia mpaka vyama vya ushirika. Hata hivyo hivi sasa Rais Saied ameamua kuvunja katiba hiyo na anadai kuwa, yeyote anayepinga uamuzi wake huo anapaswa apigwe marufuku kushiriki katika mjadala kuhusu mustakbali wa Tunisia.

Maandamano ya kupinga serikali nchini Tunisia

 

Kabla ya hapo vyama vya upinzani nchini Tunisia vilikuwa vimeapa kuwa, vitaendelea kusimama kidete kupinga vikali uamuzi ya Rais Kais Saied. Muungano huo wa vyama vya upinzani ulisisitiza kuwa, katu haukubaliani na maamuzi yanayochukuliwa na Kais Saied likiwemo tangazo lake la kuitisha kura ya maoni ya katiba au kile kinachoelezwa na rais huyo kama mageuzi ya kimsingi ya kisiasa.

Ikumbukwe pia kuwa, Kais Saied alitangaza kwa mnasaba wa Sikukuu ya Idul Fitr mwaka huu, kwamba, rasimu ya katiba mpya ya Tunisia itaandaliwa karibuni hivi na kura ya maoni itafanyika mwezi Julai. Tarehe 30 Machi mwaka huu Kais Saied alivunja bunge la Tunisia na kutishia kuwashtaki wabunge walioamua kuendesha vikao vyao mtandaoni.