May 24, 2022 07:19 UTC
  • Mbunge wa Libya: Mjumbe wa UN ni mtekelezaji wa siasa za Marekani

Muhammad al A'bani, mbunge wa Bunge la Wawakilishi la Libya amesema Stephanie Williams, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya ni mtekelezaji wa mipango na siasa za Marekani katika eneo.

Bi Williams, ambaye hapo awali alikuwa kaimu mkuu wa ofisi ya uwakilishi ya Umoja wa Mataifa mjini Tripoli, mnamo Januari 2020 aliteuliwa na Katibu Mkuu wa umoja huo Antonio Guterres kuwa mwakilishi wake maalumu katika masuala ya Libya.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Al A'bani amesema, Williams anazingatia maslahi ya Washington ambayo ni tofauti kabisa na maslahi ya taifa la Libya.

Muhammad al A'bani  ameongeza kuwa, mgogoro wa Libya hautapata ufumbuzi kwa njia inayopendekezwa na mjumbe huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya nchi hiyo.

Stephanie Williams

Pamoja na hayo, mbunge huyo amesisitiza kwa kusema, si kwamba wananchi wa Libya hawana uwezo wa kuupatia utatuzi mgogoro wa nchi yao, lakini uingiliaji wa maajinabia unaofanywa kupitia balozi zao zilizoko mjini Tripoli ndio unaokwamisha kupatikana ufumbuzi huo.

Tangu mwaka 2011 yalipofanyika mapinduzi ya wananchi yaliyopelekea kuangushwa utawala wa kiongozi wa muda mrefu Muammar Gadafi, Libya imetumbukia kwenye mapigano na machafuko yaliyochangiwa zaidi na uingiliaji wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na za eneo.../

Tags