May 24, 2022 11:14 UTC
  • Rwanda yasema raia wake wamejeruhiwa kutokana na mashambulizi ya makombora ya DRC

Jeshi la Rwanda limedai kuwa mashambulizi ya makombora katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo yaliyofanywa na Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) yamejeruhi raia kadhaa na kuharibu mali.

Taarifa ya Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) imesema shambulio hilo lililenga maeneo ya wilaya ya Musanze wakati wa asubuhi.

Kanali Ronald Rwivanga, msemaji wa RDF amesema, "Waliojeruhiwa wanapokea matibabu na maafisa wanatathmini ukubwa wa uharibifu."

Mwanamke ambaye alikuwa akirejea nyumbani kutoka kwenye bustani yake aliripotiwa kuwa miongoni mwa waliojeruhiwa.

Jeshi la Rwanda limesema limewasilisha ombi kwa Mfumo wa Uthibitishaji wa Pamoja (EJVM), ambao ni mfumo wa kijeshi wa kikanda kwa ajili ya  nchi 12 katika eneo la Maziwa Makuu, kufanya "uchunguzi wa haraka" kuhusu shambulizi hilo.

"Mamlaka za Rwanda pia zinawasiliana na wenzao wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuhusu tukio hilo," Rwivanga alisema, na kuongeza kuwa hali ni ya kawaida na usalama umehakikishwa katika eneo hilo.

Hayo yanajiri wakati ambao, hivi majuzi mapigano yalizuka kwenye milima kadhaa katika eneo la Rutshuru katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini DR Congo kati ya vikosi vya serikali na waasi wa Vuguvugu la Machi 23 (M23).

Waasi nchini DRC

Siku ya Jumapili, Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) kiliishutumu M23 kwa kushambulia kambi yake kwenye moja ya vilima vya Rutshuru, na kupelekea kikosi cha Umoja wa Mataifa kuungana na FARDC katika oparesheni ya kuwashambulia waasi.

Siku ya Jumatatu, vyombo vya habari vya ndani viliripoti kuwa mapigano hayo yalifikia eneo la mpaka kati ya DRC na Rwanda.

Mwaka 2014, Rwanda ililishutumu jeshi la DRC kwa kurusha roketi katika eneo lake katika wilaya ya mpakani ya Rubavu, magharibi mwa Rwanda.

Pia, mwaka 2013, Rwanda iliishutumu FARDC kwa kurusha makombora zaidi ya 60 katika ardhi ya Rwanda, na kuua na kuwajeruhi raia.