May 25, 2022 03:32 UTC
  • Ripoti: Rais Samia miongoni watu wenye ushawishi mkubwa duniani

Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametajwa katika orodha ya viongozi 100 wenye ushawishi mkubwa duniani.

Hayo ni kwa mujibu wa jarida la TIME 100 ambapo Samia Suluhu Hassan mwenye umri wa miaka 62 anakuwa mwanamke wa pili Mwislamu katika orodha hiyo ambapo mwingine ni mwanahabari Hoda Khamosh kutoka nchini Afghanistan

Kwa mujibu wa TIME 100 Rais Samia ametajwa katika orodha hii kutokana na uongozi wake wa kusisimua tangu alipoingia madarakani Machi 2021 na kuleta mabadiliko makubwa kwa nchi ya Tanzania ikiwemo kufungua mlango wa mazungumzo kati ya wapinzani wa kisiasa, hatua zimechukuliwa ili kujenga upya imani katika mfumo wa kidemokrasia, juhudi za kuongeza uhuru wa vyombo vya habari na amekuwa mfano wa kuigwa na wanawake na wasichana wengi.

Rais Samia Suluhu Hasasan (kulia) na Hoda Khamosh mwanahabari wa Afghanistan ni miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi duniani

 

Mnamo Septemba 2021, miezi michache ya urais wake, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa hotuba ya kihistoria kama kiongozi mwanamke wa tano pekee wa Kiafrika aliyewahi kuhutubia mkutano mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

"Kama Rais wa kwanza mwanamke katika historia ya nchi yangu," alisema, "mzigo wa matarajio ya kuleta usawa wa kijinsia ni mzito zaidi kwenye mabega yangu."

Rais Samia ameungana na marais kutoka nchi nyingine katika orodha hiyo wakiwemo Volodymir Zelenskyy wa Ukraine, Xi Jinping wa China, Vladimir Putini wa Russia na Joe Biden wa Marekani.