May 25, 2022 07:23 UTC
  • Russia yawawekea vikwazo zaidi ya wabunge 150 wa Uingereza

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imelipiza kisasi cha hatua za kiuadui zilizochukuliwa na Uingereza dhidi yake, kwa kutangaza kuwawekea vikwazo zaidi ya wabunge 150 wa Uingereza.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema katika tamko lake rasmi kuwa, Moscow imechukua hatua hiyo kujibu vikwazo vilivyowekwa na Uingereza dhidi ya wabunge 154 wa Russia.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje wa Russia imesema, Moscow imechukua hatua hiyo ili kulipiza kisasi kitendo cha kiuadui kilichotendwa na Uingereza mwezi Machi 2022 cha kuwaweka takriban wabunge wote wa Russia katika orodha ya vikwazo vyake. Kwa tangazo hilo sasa Moscow imewapiga marufuku wabunge 154 wa Uingereza kukanyaga ardhi ya Russia.

Siku zilizopita pia, Russia ilijibu vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi yake kwa kuwawekea vikwazo Wamarekani 963 na kuwaweka kwenye orodha ya watu ambao wamepigwa marufuku kukanyaga ardhi ya Russia.

Rais Vladimir Putin wa Russia

 

Hatua hiyo ya Russia ya kuwapiga marufuku wabunge 154 wa Uingereza kukanyaga ardhi ya nchi hiyo imechukuliwa katika hali ambayo tangu vilipoanza vita vya Ukraine tarehe 24 Februari 2022, London imeshaweka mamia ya vikwazo dhidi ya Russia ikiwa ni pamoja na kuzuia mali za Russia na vile vile kuwapiga marufuku watu matajiri na wanasiasa wa ngazi za juu wa Russia kuingia nchini humo akiwemo Rais Vladimir Putin.

Hivi karibuni Rais Vladimir Putin wa Russia alisema kuwa, vikwazo vya Magharibi dhidi ya Moscow kabla ya kusababisha matatizo kwa Russia vinazisababishia matatizo mengi nchi tofauti duniani zikiwemo nchi za Magharibi zenyewe, kama vile upungufu wa chakula na mfumuko wa bei za bidhaa muhimu na za dharura.

Tags