May 26, 2022 03:39 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje Somalia asimamishwa kazi kwa kuuza mkaa Oman

Waziri Mkuu wa Somalia Hussein Roble amemsimamisha kazi kwa muda Waziri wa Mambo ya Nje Abdisaid Muse Ali kutokana na hatua yake ya kuidhinisha uuzaji wa mkaa nchini Oman kinyume cha vikwazo vya kimataifa.

Umoja wa Mataifa ulipiga marufuku uuzaji wa mkaa kutoka Somalia miaka 10 iliyopita kutokana na kuwa biashara hiyo ilikuwa inatumika kufadhili kundi la kigaidi la Al Shabab, linalofungamana na al Qaeda na ambalo kwa muda mrefu limekuwa likipigana kuiangusha serikali ya Somalia.

Ofisi ya Waziri Mkuu Roble imesema ameamuru uchunguzi ufanyike kuhusu ni vipi Wizara ya Mambo ya Nje ilihusika katika kuidhinisha shehena hiyo ya mkaa iuziwe Oman.

Waziri Mkuu amebatilisha barua ya waziri wa mambo ya nje ya kuidhinisha uuzaji shehena hiyo na ametaka idara husika za serikali kufanya uchunguzi wa haraka na hatua zichukuliwe.

Waziri Mkuu wa Somalia Hussein Roble

Uuzaji mkaa ni biashara ambayo imekuwepo muda mrefu nchini Somalia. Hata hivyo mwaka 2012, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitangaza marufuku ya kimataifa ya uuzaji mkaa kutoka Somalia baada ya kubainika kuwa biashara hiyo ni chanzo kikuu cha fedha zinazotumiwa na kundi la kigaidi la al Shabab.