May 26, 2022 03:46 UTC
  • WHO: Ebola imeua watu watano nchini DRC

Shirika la Afya Duniani WHO limetangaza kuwa, watu watano wamepoteza maisha hivi karibuni kutokana na mlipuko wa 14 wa ugonjwa wa Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa mujibu wa taarifa ya WHO, tokea mlipuko mpya wa Ebola uripotiwe katika mji wa Mbandaka, katika jimbo la Equateur mnamo Aprili 23, watu 234 waliokuwa karibu na waliofariki wametambuliwa na wanachunguzwa. Aidha WHO inasema watu 1,013 wamepata chanjo ya Ebola hivi karibuni nchini DRC wakiwemo wafanyakazi 695 ambao wako mstari wa mbele kupambana na ugonjwa huo.

Mlipuko wa sasa wa Ebola nchini DRC uliripotiwa miezi minne tu baada ya mlipuko wa 13 kumalizika. Kipindi cha 2018 hadi 2020 kilikuwa na mlipuko mbaya zaidi wa Ebola nchini DRC ambapo watu 2,300 walipoteza maisha. Hivi karibuni Kenya ilitangaza hali ya tahadhari baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutangaza mlipuko mpya wa Ebola.

Chanjo ya Ebola

Daktari Samoel Khamadi, Mkurugenzi wa Kituo cha utafiti wa virusi katika Taasisi ya Matibabu ya Kenya (KEMRI) alitangaza kuwa vituo vyote vya kuingia nchini humo vimejiandaa kufanya upimaji wa virusi vya Ebola, huku idara za Afya zikifuatilia kwa makini shughuli za kuvuka mipaka ya nchi, hasusan kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Ikumbukwe kuwa, mlipuko mkubwa zaidi wa ugonjwa hatari wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone huko magharibi mwa bara la Afrika.