May 26, 2022 04:31 UTC
  • Siku ya Afrika yaadhimishwa duniani kote

Sherehe za maadhimisho ya Siku ya Afrika zimefanyika kote duniani huku kilele cha sherehe hizo kikuwa ni mkutano usio wa kawaida wa viongozi wa Afrika unaofanyika, Malabo, Guinea ya Ikweta.

Siku ya Afrika huadhimishwa kila mwaka mnamo Mei 25 kwa mnasaba wa kutiwa saini Hati ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) miaka 59 iliyopita huko Addis Ababa Ethiopia. Mnamo mwezi Julai mwaka 2002, viongozi wa nchi wanachama wa OAU walifanya kikao nchini Afrika Kusini na kuamua kubadilisha jina la jumuiya hiyo kutoka Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) na kuwa Umoja wa Afrika (AU) ambapo umoja huo sasa una wanachama 55.

AU mwaka huu inaadhimisha mwaka wa 20 tokea kuanzishwa kwake na kumepangwa sherehe maalumu kwa mnasaba huu. Mwaka huu nara na kaulimbiu ya sherehe za Siku ya Afrika ni "Kuimarisha Uthabiti Katika Lishe na Usalama wa Chakula Barani Afrika".

Kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Afrika kunafanyika mkutano usio wa kawaida wa viongozi wa Umoja wa Afrika Malabo kuanzia Jumatano hadi Jumamosi.

Chini ya uwenyekiti wa Rais Macy Sall wa Senegal ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa AU, kutakuwa na mikutano miwili ya viongozi wa nchi wanachama Ijumaa na Jumamosi. Mada kuu katika mikutano hiyo zitakuwa ni migogoro ya afya, tabianchi, chakula na usalama. Mkutano wa Jumamosi utajikita zaidi katika masuala ya vita dhidi ya ugaidi iwe ni katika Ukanda wa Sahel, Msumbiji au Somalia. Hali kadhalika viongozi wa Afrika watajadili misukosuko ya kisiasa katika nchi wanachama hasa kuibuka tena mapinduzi ya kijeshi katika eneo la Afrika Magharibi.