May 27, 2022 11:08 UTC
  • Waziri afutwa kazi Senegal baada ya watoto wachanga kuteketea kwa moto hospitalini

Rais Macky Sall wa Senegal amemfuta kazi waziri wake wa afya Abdoulaye Diouf Sarr, baada ya watoto wachanga 11 kufariki dunia kufuatia tukio chungu la moto katika chumba cha hospitali cha watoto wachanga.

Tayari Rais wa Senegela amemteua Bi Marie Khemesse Ngom kuchukua nafasi ya Abdoulaye Diouf Sarr, ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya.

Watoto wachanga 11 walifariki dunia katika ajali ya moto iliyotokea kwenye hospitali moja ya mji wa Tivaouane wa magharibi mwa Senegal.

Mamlaka za hospitali hiyo zimesema kuwa, moto huo ulisababishwa na hitilafu za umeme. Ni watoto watatu pekee ndio waliookolewa kwenye ajali hiyo ya kusikitisha.

Meya wa mji wa Tivaouane Demba Diop amesema moto huo ulisababishwa na hitilafu ya umeme na ulisambaa kwa haraka sana.

Rais Macky Sall wa Senegal

 

Siku ya Jumatano Rais Macky Sall wa nchi hiyo alituma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuelezea kusikitishwa mno na tukio hilo.

"Nimepokea kwa uchungu na kufadhaika, taarifa ya vifo vya watoto 11 wachanga vilivyotokea kwenye ajali ya moto katika kitengo cha watoto wachanga cha hospitali ya umma. Ninawapa mkono wa pole na wa masikitiko makubwa mama wa watoto hao na familia zao," ameandika Rais Sall kwenye ujumbe wake huo wa Twitter.

Tukio kama hilo lilitokea katika mji wa kaskazini wa Linguere mwishoni mwa mwezi uliopita wa Aprili, wakati moto ulipozuka hospitalini na kupelekea watoto wanne wachanga kupoteza maisha yao.