Jun 07, 2022 08:02 UTC
  • Watu 200,000 wapo katika hatari ya kufa njaa nchini Somalia

Taasisi za Umoja wa Mataifa zimesema karibu robo milioni ya wananchi wa Somalia wanakabiliwa na hatari ya kifo kutokana na baa la njaa lililosababishwa na ukame na mfumko wa bei za bidhaa kote duniani.

Taarifa ya pamoja ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), Shirika la Chakula na Kilimo la umoja huo (FAO), Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Mfuko wa Watoto wa UN (UNICEF) imeeleza kuwa, watu 213,000 wapo katika ncha ya kufa njaa, hii ikiwa ni mara tatu zaidi ya kiwango kilichotabiriwa mwezi Aprili.

Mashirika hayo ya UN yamebainisha kuwa, Wasomali milioni 7.1 (karibu nusu ya jamii ya Somalia) wanakodolewa macho na kiwango cha juu cha ukosefu wa chakula, na huenda wakalazimika kuuza mali zao ili waondokane na makali ya njaa.

Mtoto mwenye utapiamlo hospitalini Somalia

Somalia ni nchi iliyoathiriwa zaidi na ukame katika eneo la Pembe ya Afrika. Kwa uchache watu milioni 6 na laki 1 wameathiriwa na ukame, huku 771,000 kati yao wakiwa wameacha maeneo yao na kuelekea kwenye maeneo mengine kutafuta maji, chakula, na malisho.

Kwa uchache watoto milioni 1 na laki 5 wanakabiliwa na utapiamlo mkali, na zaidi ya 3,170 wameathiriwa na kipindupindu. Kesi 2,460 za surua nazo zimethibitishwa nchini humo tangu Januari. Licha ya kuongezeka mahitaji, lakini mwaka huu wa 2022 taasisi ya misaada ya kibinadamu ya Somalia kwa kifupi SHRP imesema kuwa imepokea asilimia 18 tu ya misaada inayohitajika.

Tags