Jun 12, 2022 07:55 UTC
  •  Magaidi Nigeria wawaachia huru watu 11 waliowateka katika shambulio dhidi ya treni

Abiria 11 kati ya 61 waliotekwa nyara na genge la wabeba silaha katika shambulizi la kigaidi lililolenga treni ya abiria jimboni Kaduna, Kaskazini Magharibi mwa Nigeria wameachiwa huru.

Msemaji wa timu inayofanya mazungumzo na magaidi hao, Tukur Mamu amesema abiria walioachiwa huru ni wanawake sita na wanaume watano.

Naye Sheikh Ahmad Gumi, mmoja wa viongozi mashuhuri wa kidini katika jimbo la Kaduna amesema abiria hao wameachiwa baada ya mazungumzo marefu baina yao na magaidi waliowateka nyara makumi ya abiria mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu.

Watu wasiopungua wanane waliuawa katika shambulizi hilo la kigaidi lililolenga treni ya abiria jimboni Kaduna, Kaskazini Magharibi mwa Nigeria usiku wa Machi 28.

Mwezi uliofuata wa Aprili, Shirika la Reli la Nigeria (NRC) lilitangaza kuwa, hatima ya abiria 168 haijulikani kufutia shambulizi hilo la kigaidi lililolenga treni ya abiria iliyokuwa ikitoka Abuja ikielekea Kaduna, Kaskazini mwa nchi.

Ramani inayoonesha eneo la Kaduna la kaskazini mwa Nigeria

Hilo lilikuwa shambulizi la pili la kigaidi dhidi ya treni ya abiria katika eneo hilo la nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika katika miezi ya karibuni. Hata hivyo hakuna kundi lililotangaza kuhusika na shambulizi hilo hadi sasa. 

Nchi ya Nigeria imeendelea kushuhudia mauaji na mashambulizi ya kigaidi hasa katika maeneo ya kaskazini na mashariki mwa nchi hiyo kutokana na kuweko harakati za kundi la kigaidi la Boko Haram.

Tags