Jun 15, 2022 11:56 UTC
  • Watu 1400 wameuawa katika mkoa wa Gauteng nchini Afrika Kusini

Polisi ya Afrika Kusini imesema watu zaidi ya 1,400 wameuawa katika mkoa wa Gauteng ulioko kaskazini mashariki mwa nchi katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu 2022.

Kamishna wa Polisi katika mkoa huo unaotajwa kuwa tajiri zaidi na kitovu cha fedha nchini Afrika, Luteni Jenerali Elias Mawela amesema eneo hilo limeshuhudia ongezeko la mauaji kwa asilimia 45.2 ndani ya robo ya kwanza ya mwaka huu, ikilinganishwa na kipindi kama hicho katika mwaka 2020/2021.

Jenerali Mawela ameeleza kuwa, akthari ya mauaji yanayoshuhudiwa kwenye mkoa huo ambao una mji mkuu wa Afrika Kusini, Pretoria na jiji kubwa zaidi nchini humo Johannesburg, yametokana na visa vya ufyatulianaji risasi, ugomvi, kutoelewana na malumbano yanayosababishwa na ajali za barabarani.

Mawela amebainisha kuwa, mauaji hayo hayatokani na ugomvi wa kinyumbani, na kwamba aghalabu yake yanachangiwa na ulevi wa kupindukia na utumiaji wa mihadarati.

Washukiwa wa uhalifu Afrika Kusini

Kamishna wa Polisi katika mkoa wa Gauteng ulioko kaskazini mashariki mwa Afrika Kusini ameongeza kuwa, jinai za kingono zimeongezeka pia katika mkoa huo kwa asilimia 11.3, ambapo visa 2,921 vimeripotiwa, vikiwemo 2,267 vya ubakaji.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi punde za Jeshi la Polisi la Afrika Kusini, kwa wastani watu 67 wanauawa kila siku katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

 

Tags