Jun 22, 2022 11:48 UTC
  • Kiongozi wa wanajeshi wafanya mapinduzi Burkina Faso akutana na rais aliyepinduliwa

Kiongozi wa wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini Burkina Faso amekutana na rais aliyeondolewa madarakani katika mapinduzi yaliyofanyika mapema mwaka huu. Kiongozi wa mapinduzui ya kijeshi ya Burkina Faso amekutana na Roch Marc Christian Kabore katika juhudi za kujaribu kutuliza hali ya kisiasa nchini humo.

Rais wa zamani wa Burkina Faso, Roch Marc Christian Kabore aliyekuwa madarakani hadi alipopinduliwa mwezi Januari mwaka huu alifuatana na rais mwingine wa zamani wa nchi hiyo Jean-Baptiste Ouedraogo katika mazungumzo hayo yaliyofanyika ikulu ya rais. Ouedraogo alishika hatamu za uongozi kuanzia Novemba mwaka 1982 hadi Agosti 1983. 

Bwana Kabore alisalimiana kwa kupeana mkono na Luteni Kanali Paul- Henri Sandaogo Damiba na ripoti zinasema wawili hao walifanya mazungumzo katika anga tulivu.

Ofisi ya wanajeshi wanaoongoza Burkina Faso imesema kuwa pande tatu zimejadili masuala ya usalama, namna ya kusimamia kipindi cha mpito na masuala mengine yenye maslahi kwa taifa. Taarifa hiyo aidha imeeleza kuwa, viongozi hao wamedhihirisha hamu ya kufikia mapatano, kuwa na Burkina Faso yenye umoja, azma ya kweli na inayounga mkono vita dhidi ya ugaidi.

Luteni Kanali Paul-Henri Damiba 

Sawa na inavyoshuhudiwa huko Mali na katika nchi jirani ya Niger, Burkina Faso pia imekuwa mhanga wa machafuko na mashambulizi ya makundi ya wanamgambo wenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida na Daesh. 

Utawala mpya wa Burkina Faso unaoongozwa na Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba umeahidi kurejesha amani huku ukimlaumu kiongozi aliyeondolewa madarakani, Marc Kabore, kwa kushindwa kuchukua hatua za kutosha za kukabiliana na makundi ya kigaidi. 

Tags