Jun 23, 2022 07:57 UTC
  • Ndoa za utotoni Sudan Kusini zaendelea kuwa changamoto kwa jamii ya nchi hiyo

Ripoti zinasema kuwa, baadhi ya mabinti wadogo nchini Sudan Kusini wangali wanapigwa mnada kuingia katika ndoa mkabala wa waoaji kutoa mahari ya mifugo ya ng'ombe kwa familia za mabinti wanaoolewa.

Ndoa hizo za utotoni zimetajwa kuwa moja ya changamoto zinazoikabili jamii ya watu wa Sudan Kusini. Bei ya binti anayepaswa kuolewa inategemea na mazungumzo yatakayofikiwa kati ya baba yake na muoaji na kuanzia ng'ombe 50 hadi 100. Kila ng'ombe hukadiriwa kuwa na thamani ya dola elfu moja. Binti ambaye ataonekana kuwa mrembo, aliyenona na wa tabaka la juu ana uwezo wa kupatiwa familia yake ng'ombe nyingi zisizopungua 200. Kesi moja ya binti ambayo ilivuma sana miaka kadhaa iliyopita huko Sudan Kusini ilihusiana na binti aliyeolewa ambapo muoaji alitoa ng'ombe wapatao 520 pamoja na magari kadhaa. 

Jackline Nasiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Utawala Shirikishi, Amani na Haki katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba anasema kuwa, kadiri mtoto wa kike anavyokuwa mdogo ndivyo familia yake inavyopokea ng'ombe wengi mkabala wake. "Wanauza mabinti zao ili kupata fedha za kuendesha maisha." Uhuru wa Sudan Kusini uliopatikana mwaka 2011 ulitoa matumaini makubwa kwa jamii ya watu milioni 12 wa nchi hiyo ya kurejea amani na kuboresha hali ya maisha hata hivyo ni hatua chache tu ndizo zimechukuliwa na serikali ya Juba katika uwanja huo.

Ndoa za utotoni ni changamoto kuu Sudan Kusini 

Nchi hiyo changa zaidi duniani aidha ilitumbukia katika vita vya ndani vilivyodumu kwa miaka mitano na kisha kufikiwa makubaliano ya amani yenye kulegalega mwaka 2018. Mizozo na mapigano ya ndani aidha yanaendelea kuitatiza Sudan Kusini huku watu wengi wa nchi hiyo wakisalia katika dimbwi la umaskini.

Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa limetoa takwimu zinazoonyesha kuwa, Sudan Kusini ni nchi ya tano duniani kwa visa vya  ndoa za utotoni. 

 

Tags