Jun 23, 2022 12:21 UTC
  • Wakazi wa mashariki ya DRC wakataa kikosi cha EAC kupelekwa eneo hilo

Baadhi ya wakazi wa eneo la mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamelikataa pendekezo la kupelekwa katika eneo hilo askari wa kulinda amani kutoka nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki.

Siku ya Jumatatu, viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) waliokutana mjini Nairobi, Kenya waliidhinisha uamuzi wa kupeleka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kikosi cha askari kutoka nchi wanachama wa EAC ili kusaidia kurejesha amani na uthabiti mashariki ya nchi hiyo. 

Hatua hiyo ilikuwa imeshajadiliwa hapo kabla na wakuu wa majeshi ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Hata hivyo baadhi ya Wakongomani wa eneo la maashariki ya DRC wamepinga mpango huo kwa hoja kwamba baadhi ya nchi jirani zitakazoshirikishwa kwenye kikosi hicho zina rekodi ya kujihusisha na vita vya ndani ya nchi hiyo.

Wakazi hao wa mashariki ya DRC wametaka badala yake vifanyiwe mageuzi na kuimarishwa vikosi vya jeshi la nchi hiyo FARDC.

Vuguvgu la kupigania mabadiliko la raia wa DRC liitwalo Lucha, limeeleza katika barua yake kwa Rais wa nchi hiyo Felix Tshisekedi kwamba, linalikataa pendekezo hilo kwa sababu za kiusalama, kiuchumi au kijiopolitiki na kumtolea mwito kiongozi huyo wa kumtaka aachane nalo.

Vuguvugu hilo la Lucha lililoasisiwa miaka kumi iliyopita katika mji wa Goma, makao makuu ya mkoa uliogubikwa na machafuko wa Kivu Kaskazini ambao unapakana na Rwanda na Uganda, limefafanua katika barua yake kwamba, kwa akali, wanachama watatu kati ya saba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, yaani Rwanda, Uganda na Burundi zimejihusisha kwa zaidi ya miongo miwili katika kuvuruga uthabiti wa Kongo DR, kwa kujiingiza moja kwa moja kupitia majeshi yao au kupitia makundi yanayobeba silaha.

Nchi hizo tatu zinazopakana na DRC katika upande wake wa mashariki zilijihusisha na kuingilia vita vya ndani vilivyotokea mara mbili kati ya 1996 na 2003 katika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini.

Mbali na upinzani wa wakazi wa eneo la mashariki ya DRC, serikali ya Kinshasa imeeleza bayana kuwa inapinga ushiriki wa Rwanda katika kikosi cha nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki, ikiituhumu nchi hiyo kuwa inawasaidia na kuwaunga mkono waasi wa M23, tuhuma ambazo Kigali inazikanusha.../

Tags