Jun 24, 2022 01:16 UTC
  • Afrika Kusini yasajili kesi ya kwanza ya ugonjwa wa Monkeypox

Afrika Kusini imeripoti kesi ya kwanza iliyothibitishwa ya ugonjwa wa virusi wa Monkeypox.

Dakta Joe Phaahla, Waziri wa Afya wa Afrika Kusini amesema aliyegunduliwa kuwa na maradhi hayo ni mwanaume wa miaka 30 anayeishi katika mkoa wa Gauteng ulioko kaskazini mwa nchi. Amesema mtu aliyepatikana na maradhi hayo hana historia ya kusafiri nje ya nchi, ikiwa na maana kuwa kesi hiyo iliyoripotiwa ni ya ndani ya nchi.

Amesema Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza (NICD) ipo mbioni kumfuatilia mgonjwa huyo, ili ijue ametangamana na kina nani na iwapo waliotangamana naye wameambukizwa au la.

Mripuko wa sasa wa ugonjwa huo unaoshabihiana na Ndui umelipiga zaidi bara Ulaya, na hususan nchi za Uingereza, Uhispania, Ujerumani, Ureno na Ufaransa. Aidha kesi kadhaa za maradhi hayo zimeripotiwa nchini Marekani na Canada.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mbali na Afrika Kusini, nchi nyingine 8 za Afrika ni miongoni mwa nchi 40 duniani zilizoripoti kesi za ugonjwa wa Monkeypox.

Dakta Joe Phaahla, Waziri wa Afya wa Afrika Kusini

Nigeria ndiyo inayoongoza barani Afrika kwa kuwa na kesi nyingi za maradhi hayo, ambapo hadi sasa taifa hilo la Afrika Magharibi limeripoti kesi 36, likifuatia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo-kesi 10, huku Benin ikishika nafasi ya tatu barani humo kwa kunakili kesi 8.

WHO imesema nchi mbili za Afrika ambazo hazijawahi kuwa na historia ya kusajili kesi za mara hayo huko nyuma ni Ghana, ambayo hivi sasa imerekodi kesi 5 na Morocco kesi moja.

Aidha kuna kesi zinazoshukiwa kuwa za maradhi hayo katika nchi za Ethiopia, Guinea, Liberia, Msumbiji, Sierra Leone, Sudan na Uganda.

Tags