Jun 24, 2022 01:17 UTC
  • Hatima ya Sheria za Kiislamu Nigeria kujulikana kabla ya Oktoba

Mahakama moja nchini Nigeria jana Alkhamisi iliakhirisha uamuzi wake kuhusu shauri lililowasilishwa mbele yake likipinga utekelezwaji wa Sheria za Kiislamu (Sheria) katika jimbo la Kano la kaskazini mwa nchi.

Shauri hilo liliwasilishwa na mwanamuziki Yahaya Aminu Sharif, akikata rufaa dhidi ya hukumu ya kifungo cha miaka 10 jela kwa kupatikana na hatia ya 'kukufuru' iliyotolewa mwaka 2020 na Mahakama ya Sheria za Kiislamu jimboni Kano.

Wakili wa mwanamuziki huyo mwenye miaka 22, Kola Alapinni aliitaka Mahakama imuachie huru kijana huyo, sambamba na kutangaza kuwa Sheria za Kiislamu zinakiuka Katiba ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Waendesha Mashitaka wa Serikali jimboni Kano wameitaka mahakama hiyo itupilie mbali rufani iliyowasilishwa na wakili wa Yahaya, na ishikilie hukumu ya Mahakama Kuu ya kutaka kesi hiyo isikilizwe upya. Wanasisitiza kuwa, hakuna kipengee chochote cha Sheria za Kiislamu kinachokanyaga moyo wa Katiba.

Polisi wa Kiislamu 'Hisbah' jimboni Kano wakiharibu pombe

Majaji watatu walioisilikiza kesi hiyo wamesema watatoa uamuzi wao juu ya faili hilo kabla ya mwezi Oktoba mwaka huu 2022. Uamuzi huo una umuhimu mkubwa kwa kuwa utaainisha hatima ya utekelezwaji wa Sheria za Kiislamu nchini Nigeria.

Jimbo la Kano ni moja kati ya majimbo ya Kaskazini mwa Nigeria ambayo yanafuata Sheria za Kiislamu (Sharia) tangu mwaka 2000, lakini wanazingatia pia sheria za nchi. Akthari ya wakazi wa maeneo ya Kaskazini mwa Nigeria ni Waislamu.

Tags