Jun 24, 2022 03:14 UTC
  • WFP: Maisha ya Waethiopia milioni 20 yako hatarini kutokana na vita, ukame na uhaba wa chakula

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limetahadharisha kuwa, baa la njaa linazidi kutishia maisha ya Waethiopia milioni 20 ambao wanakabiliwa na vita kaskazini mwa nchi hiyo, ukame katika eneo la kusini na kupungua kwa msaada wa chakula na lishe kuanzia mwezi ujao.

Indhari hiyo iliyotolewa na WFP imebainisha kuwa,  mchanganyiko wa migogoro na ukame umesababisha ongezeko la mfumuko wa bei; na hadi mwezi Aprili mwaka huu mwelekeo wa bei ya chakula nchini Ethiopia ulipanda kwa asilimia 43 ikilinganishwa na mwezi kama huo mwaka jana. Wakati huo huo, bei za mafuta ya mboga na nafaka zimekuwa zikipanda kwa zaidi ya asilimia 89 na asilimia 37 mwaka hadi mwaka.

Kwa mujibu wa shirika hilo la UN, miezi 19 ya vita imewaacha zaidi ya watu milioni 13 kaskazini mwa taifa hilo la Pembe ya Afrika wakihitaji msaada wa kibinadamu wa chakula, hasa katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro katika majimbo ya Afar, Amhara na Tigray. 

WFP imebainisha pia kwamba, katika eneo la Tigray, zaidi ya asilimia 20 ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, na nusu ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha, wana utapiamlo. 

Msafara wa WFP ukiwa na msaada wa vyakula kwa ajili ya watu wa maeneo ya Tigray na Afar

Aidha katika maeneo ya kusini na kusini-mashariki mwa Ethiopia, wastani wa watu milioni 7.4 huamka na njaa kila siku wakati nchi ikikabiliana na msimu wa nne mfululizo wa kutokuwa na mvua mtawalia.

Shirika hilo la UN limeeleza pia kwamba, athari mbaya za vita nchini Ukraine zinatarajiwa kuzidisha mzozo wa uhakika wa chakula nchini Ethiopia. 

Wakati zaidi ya robo tatu ya msaada wa WFP na ngano ya serikali ambayo ni chakula kikuu nchini Ethiopia inatoka Ukraine au Urusi, vita vinatishia kuongeza gharama yake pamoja na ile ya mbolea, hali ambayo iko nje ya uwezo wa mamilioni ya wakulima wa Ethiopia.../

 

Tags