Jun 24, 2022 14:26 UTC
  •  Michelle Bachelet
    Michelle Bachelet

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa sambamba na kulaani mauaji ya halaiki ya hivi karibuni ya raia hususan wanawake na watoto wadogo magharibi mwa Ethiopia, ameitaka serikali ya Addis Ababa kufanya uchunguzi huru, wa kina, wa haraka na usioegemea upande wowote.

Katika taarifa, Michelle Bachelet amesema: Nimeshtushwa mno na mauaji hayo yasiyo ya kiutu na idadi kubwa ya watu kufurushwa kwenye makazi yao katika kijiji cha Tole.

Ofisa huyo mwandamizi wa UN amezitaka mamlaka za Ethiopia kufanya uchunguzi wa kina, na kuhakikisha kuwa familia za wahanga wa shambulio hilo lililopelekea kuuawa mamia ya watu katika eneo la Oromia zinapata haki, kwa kuwajibishwa wahusika, kufamishwa ukweli juu ya shambulio hilo, na pia kupewa fidia.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, watu kati ya 260 na 320, wengi wao kutoka kabila la Amhara, waliuawa katika shambulio hilo lililofanyika katika eneo la Oromia ambalo akthari ya wakazi wake ni watu wa jamii ya Oromo.

Eneo la Oromia kwenye ramani ya Ethiopia

Mashuhuda walisema wapiganaji wa Jeshi la Ukombozi wa Oromo (OLA) ndio waliohusika na shambulizi hilo ambalo linahesabiwa kuwa moja ya mashambulizi mabaya zaidi katika kumbukumbu za miaka ya hivi karibuni.

Inaarifiwa kuwa, watu zaidi ya elfu mbili walilazimishwa kuyahama makazi yao katika kijiji cha Tole eneo la Oromia, wakati wa hujuma hiyo ya kikatili Jumamosi iliyopita.

Tags