Jun 25, 2022 11:47 UTC
  • Morocco: Wahajiri 18 wameaga dunia wakijaribu kuingia eneo la Melilla la Uhispania

Serikali ya Morocco imesema wahajiri 18 wamepoteza maisha, huku makumi ya wengine pamoja na askari polisi wakijeruhiwa katika mkanyagano wa kujaribu kuingia katika maeneo ya Melilla na Ceuta yanayodhibitiwa na Uhispania.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco imesema wahajiri hao waliaga dunia kwa kukanyagana walipokuwa wanajaribu kuruka uzio wa chuma unaoyatenganisha maeneo hayo mawili, huko kaskazini mwa Morocco.

Taarifa ya wizara hiyo imesema wahajiri watano waliaga dunia katika eneo la tukio, huku wengine 13 wakifariki dunia hospitalini wakitibiwa. Imeongeza kuwa, wahajiri wengine 76 na maafisa usalama wa Morocco wapatao 140 wamejeruhiwa kwenye mkanyangano huo.

Hata hivyo Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Morocco limeripoti kuwa, walioaga dunia kwenye mkasa huo wa jana Ijumaa ni wahajiri 27, akthari yao wakiwa ni raia wa nchi za eneo la chini ya Jangwa la Sahara barani Afrika.

Wahajiri katika uzio unaotenganisha Melillah na Morocco

Naye msemaji wa ofisi ya serikali ya Uhispania mjini Melilla amesema wahajiri karibu 2,000 mapema jana Ijumaa walijaribu kuingia katika eneo hilo linalodhibitiwa na Uhispania kaskazini mwa Morocco, na kwamba kundi moja kubwa la wahajiri wapatao 130 wa Kiafrika limefanikiwa kuingia kwenye eneo hilo kinyume cha sheria.

Miji ya Melilla na Ceuta ina utawala wa ndani na iko chini ya serikali ya Uhispania licha ya kwamba kijiografia iko kaskazini mwa Morocco. Miji hiyo ndio mpaka pekee wa ardhini baina ya bara la Afrika na nchi za Ulaya. 

Tags