Jun 26, 2022 11:18 UTC
  • Vita vimewatenganisha mamia ya watoto na familia zao DRC

Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Uganda limesema mamia ya watoto wamelazimika kutengana na wazazi na jamaa zao kutokana na mapigano huko mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Abel Nuwamanya, ofisa wa Msalaba Mwekundu nchini Uganda amesema shirika hilo linawahudumia watoto 700 wenye umri kati ya miaka 5 na 17, ambao wamepoteza mawasiliano na jamaa zao kutokana na makabiliano yanayoendelea baina ya wanajeshi wa serikali ya DRC na kundi la waasi la M23.

Ameeleza kuwa, watoto hao wapo katika kambi ya wakimbizi ya Nyakabade iliyoko karibu na mpaka wa Uganda na Kongo DR, na kwamba wengine 100 wapo katika uangalizi wa Shirika la Msalaba Mwekundu DRC.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), machafuko ya tangu Machi mwaka huu yamesababisha takriban watu 158,000 kuyahama makazi yao katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Hali mbaya ya wakimbizi wa DRC kambini

OCHA imesema aghalabu ya waliokimbia makazi yao ni wanawake na watoto kutoka maeneo ya Rutshuru na Nyiragongo huko Kivu Kaskazini, mpakani mwa Uganda na Rwanda.

Kuibuka tena kwa kundi la waasi la M23 mwezi Machi mwaka huu, ni chanzo kikuu cha ukosefu wa usalama katika mkoa wa Kivu Kaskazini. Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki hivi karibuni ziliidhinisha mpango wa kutumwa kikosi cha askari wa kieneo kwenda kukabiliana na waasi huko mashariki mwa DRC.

Tags