Jun 26, 2022 11:18 UTC
  • Maiti 17 zapatikana kwenye ukumbi wa starehe Afrika Kusini

Polisi ya Afrika Kusini inachunguza vifo vya kutatanisha vya watu 17 kwenye ukumbi mmoja wa starehe katika mji wa East London, kusini mashariki mwa nchi.

Brigedia Thembinkosi Kinana, Msemaji wa Polisi katika eneo la Eastern Cape amesema wameanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha vifo vya watu hao katika klabu ya starehe ya Enyobeni mjini East London.

Naye Msemaji wa Idara ya Afya eneo la Eastern Cape, Siyanda Manana amesema miili ya watu hao imepelekwa katika hifadhi ya maiti ya serikali ya Woodbrook katika eneo hilo.

Amezitaka familia za watu hao kwenda kuwatambua wapendwa wao waliouawa au kufariki dunia katika mazingira ya kutatanisha, huku uchunguzi wa kina ukiendelea.

Awali duru mbalimbali za kuaminika zilikuwa zimesema kuwa, idadi ya maiti zilizopatikana kwenye eneo la tukio ni 22. Mashuhuda wanasema waliouawa wanaonekana kuwa vijana wenye umri kati ya miaka 18 na 22.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, vijana hao walikusanyika jana usiku kwenye ukumbi huo wa starehe wakiwa wamevalia mavazi meusi, kwa ajili ya sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa wawili miongoni mwao.

Tags