Jun 29, 2022 04:00 UTC
  • UN: Uchunguzi ufanyike kuhusu mauaji ya Waafrika mpakani mwa Morocco na Hispania

Umoja wa Mataifa umesikikitishwa na vifo vya Waafrika 23 na wengine zaidi ya 76 kujeruhiwa wakati wakijaribu kuvuka mpaka kati ya Morocco na Hispania ili kwenda barani Ulaya kupitia mpaka wa Mellila na Ceuta.

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Ravina Shamdasani akiwa mjini Geneva Uswisi imesema tukio hilo lililotokea tarehe 24 Juni 2022 linapaswa kuchunguzwa kwa makini na nchi zote mbili na wote waliosababisha vifo na majeruhi wachukuliwe hatua za kisheria na wawajibishwe kama inavyofaa.

Shamdasani amewaambia waandishi wa habari kuwa hii ni idadi kubwa zaidi ya vifo vya wahamiaji kurekodiwa katika tukio moja baada ya miaka mingi na kwamba “ofisi ya haki za kinadamu imepokea ripoti za wahamiaji hao kuchapwa na fimbo, kupigwa mateke, kushambuliwa na mawe pamoja na kurushwa na maafisa wa Morocco wakati wakijaribu kuinua waya wenye urefu wa takriban mita sita mpaka kumi ambao unatenganisha Morocco na Melilla.”

Amesema katika harakati hizo za kuwazuia Waafrika hao kuvuka askari wa mpakani wa Morocco mia moja na arubaini nao wameripotiwa kupata majeraha.

Wahajiri waliouawa wakijaribu kuinga Uhispania

“Tunatoa wito kwa Morocco na Hispania kuhakikisha wanaheshimu haki za binadamu za wahamiaji katika mpaka wao wa pamoja na maafisa walio mpakani waepuke matumizi yoyote ya nguvu kupita kiasi dhidi ya wahamiaji.” Amesema Shamdasani

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia imetaka hatua zote za haraka zichukuliwe kupitia Jumuiya ya Ulaya, Umoja wa Afrika pamoja na wahusika wengine wa kimataifa na kikanda katika kuhakikisha mipakani kuna utawala bora unaozingatia haki za binadamu. “Hatua hizo ni pamoja na kuhakikisha kuna njia salama za wahamiaji kupita, kufanyika kwa tathmini binafsi za kila mtu anayetaka kupita mpakani, pamoja na kuwahakikishia ulinzi dhidi ya kufukuzwa kwa pamoja au kukamatwa na kuwekwa vizuizini kuholela”.