Jun 29, 2022 10:26 UTC
  • Mahakama ya Misri yatoa hukumu ya kifo kwa wanamgambo 10

Mahakama moja ya Misri imewahukumu kifo wanamgambo 10 waliopatikana na hatia inayohusiana na vitendo vya ugaidi.

Wanaume hao ambao walishtakiwa kwa kuongoza kundi lijulikanalo kama Helwan Brigades, walikutwa na hatia ya kufanya vitendo vya ugaidi, ikiwemo kufyatua risasi kwenye gari la polisi.

Watu hao wamehukumiwa kuhusiana na matukio ya kati ya Agosti 2013 na Februari 2015, kipindi ambacho kulifanyika mashambulizi mengi, yaliyolenga haswa maafisa wa usalama, kufuatia Jeshi kumuondoa madarakani rais mwenye itikadi za Kiislamu Mohamed Morsi.

Mrengo wa harakati ya Ikwanul Muslimin ujulikanao kama Brigedi za Helwan unalaumiwa kutekeleza mashabulizi hayo.

Mahakama iliwapunguzia pia vifungo vya jela watuhumiwa wengine 205 katika kesi hiyo, baadhi wakihukumiwa miaka 10 jela wengine kifungo cha maisha.

Rais Abdel Fattah Al-Sisi wa Misri

Mufti wa Misri anatakiwa kuidhinisha hukumu ya kifo kabla haijatekelezwa ingawa wakati mwingine mahakama huwa na haki ya kupuuza maoni yake.

Tangu aingie madarakani mwaka wa 2014, mwaka mmoja baada ya kuongoza kuondolewa madarakani kwa Morsi, Rais Abdel Fattah Al-Sisi ameongoza kwa kufanya ukandamizaji mkali dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu na wapinzani, na kuwatia jela maelfu.