Jun 30, 2022 02:22 UTC
  • Umoja wa Afrika watuma waangalizi wa uchaguzi nchini Kenya

Umoja wa Afrika (AU) umetuma waangalizi kufuatilia uchaguzi mkuu wa Agosti 9 nchini Kenya ambao umepelekea joto la kisiasa kupanda nchini humo.

Taarifa ya Umoja wa Afrika imesema, “Kufuatia mwaliko wa Serikali ya Jamhuri ya Kenya kwa Umoja wa Afrika kuangalia uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Agosti 9, 2022, Tume ya Umoja wa Afrika inatuma ujumbe wa wataalamu wa kimataifa wa uchaguzi nchini Kenya unaojumuisha wataalamu wa timu nane."

Timu hizo zinapaswa kutathmini maandalizi ya uchaguzi wa Kenya, mienendo ya kisiasa na usawa wa kampeni za uchaguzi.

Umoja wa Afrika umesema, "Timu kuu itafuatilia maandalizi ya uchaguzi, kutathmini mienendo ya kisiasa na ushindani wa kweli na usawa wa kampeni ya uchaguzi, na kudumisha mawasiliano ya mara kwa mara na wadau wa kitaifa na kimataifa kabla, wakati na baada ya uchaguzi."

AU pia itatuma timu nyingine ya waangalizi wiki chache kwenye uchaguzi, na baadaye waangalizi wengine wengi wa muda mfupi wiki moja kabla ya siku ya uchaguzi.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Kenya Wafula Chebukati

Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki (COMESA)  mapema mwezi Mei zilituma ujumbe wa pamoja wa tathmini ya kabla ya uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi usio na ghasia, haki na wa kuaminika ambao utaimarisha mchakato wa kidemokrasia nchini Kenya.

Washindani wakuu katika uchaguzi huo ni Raila Odinga wa Muungano wa Azimio na Naibu wa Rais William Ruto wa muungano wa Kenya Kwanza. Mara hii Odinga anaungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta kufuatia mapatano ya wawili hao Machi 2018 maarufu kama handisheki na ana matumaini makubwa kuwa uungaji mkono wa serikali iliyopo madarakni utamuwezesha kushinda. Mapatano hayo ya Odinga na Kenyatta yalipelekea kutengwa Naibu Rais William Ruto katika shughuli za kiserikali.