Jun 30, 2022 08:12 UTC
  • AU yataka Sudan, Ethiopia ziache makabiliano ya kijeshi mpakani

Kamisheni ya Umoja wa Afrika imetoa mwito kwa nchi za Sudan na Ethiopia kujizuia na kutochukua hatua yoyote inayoweza kushadidisha mivutano ya kijeshi katika eneo la al-Fashaqa, lililoko katika mpaka wa pamoja wa nchi mbili hizo jirani.

Taarifa ya kamisheni hiyo imesema mwenyekiti wake, Moussa Faki Mahamat anafuatilia kwa wasiwasi mkubwa hatua ya kuongezeka mgogoro wa kijeshi katika mpaka wa nchi mbili hizo.

Mwenyekiti huyo wa Kamisheni ya AU katika taarifa hiyo ameyataka mataifa hayo mawili kusuluhisha mgogoro uliopo kwa njia za amani na diplomasia.

Haya yanajiri baada ya majeshi ya Sudan kufyatua mizinga mikubwa wakati wa mapigano katika eneo la mashariki linalozozaniwa la al-Fashaqa linalopakana na Ethiopia.

Mzozo kuhusu eneo la al-Fashaqa, ambalo lipo ndani ya mipaka ya kimataifa ya Sudan lakini limekaliwa na wakulima wa Ethiopia kwa miongo kadhaa sasa, umeongezeka katika miaka ya hivi karibuni sambamba na mzozo wa kidiplomasia kuhusu ujenzi wa Ethiopia wa bwawa la kufua umeme wa maji.

Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU

Jumanne Sudan iliweza kuteka eneo la Jabal Kala al-Laban, lililo karibu na mpaka huo unaozozaniwa, kufuatia shambulio la anga, kwa mujibu wa afisa wa  kijeshi wa Sudan ambaye hakutajwa jina akizungumza na shirika la habari la Reuters.

Siku ya Jumatatu, Ethiopia ilikanusha tuhuma za Khartoum kwamba jeshi lake lilikamata na kuwanyonga wanajeshi saba wa Sudan na raia mmoja, na badala yake ikasema mauaji hayo yametekelezwa na wanamgambo wa eneo hilo.

Duru za serikali ya Sudan zilisema kuwa Sudan imewasilisha malalamiko rasmi kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji hayo.

Tags