Jun 30, 2022 13:29 UTC
  • Wasudani waandamana  dhidi ya utawala wa kijeshi katika maadhimisho ya mapinduzi yaliyomng'oa al Bashir

Umati mkubwa wa watu, makundi kwa makundi, wameandamana leo dhidi ya utawala wa kijeshi nchini Sudan na kukabiliwa na gesi ya kutoa machozi kutoka kwa vikosi vya usalama vya nchi hiyo. Huduma za mawasiliano zilikatwa wakati wa maandamano hayo mapema leo katika mji mbalimbali ya Sudan.

Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miezi kadhaa ambapo wananchi wa Sudan wanaandamana wakipinga utawala wa kijeshi ulioko madarakani huku huduma za intaneti na simu zikiwa zimekatwa, na askari jeshi wakiwa wamejizatiti kwa silaha katika maeneo mbalimbali. 

Wananchi wa Sudan wamefanya maandamano hayo leo Alkhamisi kuadhimisha kutimia mwaka wa tatu ambapo maandamano makubwa mtaliwa yalifanyika nchini humo  mwaka 2019 na kupelekea kuondolewa madarakani mtawala wa muda mrefu, Omar al Bashir.

Baada ya kupinduliwa Omar Hassan al Bashir huko Sudan mwaka 2019, kuliasisiwa serikali ya mpito  kati ya makundi ya kiraia na jeshi. Hata hivyo mwezi Oktoba mwaka jana, jeshi la Sudan likiongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan, liliipindua serikali hiyo ya mpito na kuchochea maandamano makubwa ya upinzani ambayo yamekuwa yakilitaka jeshi liachane na siasa za Sudan. 

Abdel Fattah al Burhan, mtawala wa kijeshi wa Sudan 

Habari zinasema kuwa, katikati ya Khartoum, mji mkuu wa Sudan, vikosi vya usalama vimewanyunyuzia waandamanaji gesi ya kutoa machozi na maji washa ili kuwazuia kuelekea katika ikulu ya rais. Baadhi ya waandamanaji walikuwa wamebeba mabango yanayosomeka: "haki itendeke kwa wale wote waliouliwa katika maandamano", huku mabango mengine yakiwa na maandishi yasemayo" Burhan, Burhan rudi kambini na kabidhi kampuni unazomiliki", ikiwa ni ishara ya namna viongozi wa jeshi la Sudan walivyohodhi uchumi wa nchi hiyo.