Jun 30, 2022 13:32 UTC
  • Mjumbe wa UN Kongo alitahadharisha Baraza la Usalama kuhusu hali ya usalama Kongo

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Bintou Keita amelitahadharisha Baraza la Usalama la umoja huo kuhusu machafuko ambayo yanaweza kuibuka mashariki mwa nchi hiyo ambako makundi ya wanamgambo wenye silaha yanaongezeka kila siku.

Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama la UN, Bintou Keita amesema kuwa, iwapo kundi la waasi wa M23 litaendeleza mashambulizi yake dhidi ya vikosi vya ulinzi vya Kongo na MONUSCO, basi kikosi hicho cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kitajikuta kikikabiliwa na tishio zaidi ya uwezo wake. 

Ameongeza kuwa, harakati za kundi la M23 na makundi mengine ya waasi huko mashariki mwa Kongo zinatishia kurudisha nyuma mafaniko na hatua zilizopigwa kwa bidii kubwa za kurejesha amani na utulivu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.  

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa amelitaka Baraza la Usalama kuingilia kati katika kadhia ya  Kongo DR na Rwanda ili zifikie mapatano baada ya kuibuka mvutano kati ya nchi mbili hizo. 

Bintou Keita, Mjumbe wa UN Kongo 

Wakati huo huo Bintou Keita amezungumzia kikosi cha kulinda amani cha kikanda ambacho nchi kadhaa za Mashariki mwa Afrika zinataka kitumwe huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kutilia mkazo umuhimu wa kushirikiana kikosi hicho kipya na MONUSCO sambamba na kuainisha majukumu ya kuwalinda raia na kuheshimu haki za binadamu wakati utendaji wa kikosi hicho. 

Amesema, sehemu ya kikosi hicho kipya inatarajiwa kutumwa mashariki mwa Kongo kabla ya mwisho wa mwezi Julai mwaka huu na askari wengine watakuwa huko mwezi Agosti.

Tarehe 20 mwezi huu viongozi wa Afrika Mashariki walikubaliana kuunda kikosi cha kikanda ili kujaribu kuhitimisha mzozo baina ya Kigali na Kinshasa huko mashariki mwa Kongo.

Tags