Jul 01, 2022 08:03 UTC
  • Rais wa Tunisia azindua rasimu ya katiba mpya ya nchi hiyo inayopingwa na wengi

Rais Kais Saeid wa Tunisia amezindua rasimu ya katiba mpya ya nchi hiyo ambayo ndani yake inashuhudiwa kwa uwazi jinsi rais huyo alivyoongezewa mamlaka ya utawala.

Rasimu ya katiba mpya ya Tunisia imepangwa kupigiwa kura ya maoni tarehe 22 ya mwezi huu wa Julai.

Ripoti kutoka Tunis, mji mkuu wa Tunisia zinasema, imeelezwa katika rasimu hiyo kwamba, kwa msaada wa baraza la mawaziri, rais atakuwa ndiye mkuu wa mhimili wa serikali.

Kwa mujibu wa rasimu hiyo ya katiba mpya ya Tunisia, uteuzi wa majaji, nao pia hautawezekana kufanywa bila ya amri ya rais.

Lakini mbali na hayo, kulingana na rasimu ya katiba mpya, kutakuwapo pia na mabunge mawili ambayo ni bunge la wawakilishi na bunge la baraza la taifa, lakini miswada ya mabunge yote hayo mawili haitakuwa sheria ila baada ya kusainiwa na rais.

Maandamano ya kupinga hatua za Rais Kais Saeid

Mnamo Juni 25 mwaka jana, rais Kais Saeid alihodhi madaraka ya nchi kwa kutekeleza hatua kadhaa za aina yake ikiwemo kulisimamisha Bunge na kumfuta kazi spika wake, pamoja na waziri mkuu wa serikali, na kuchukua udhibiti wa mambo yote ya nchi. Hatua ya Rais Saed ya kuifuta kazi serikali ilisababisha mkwamo mkubwa wa kisiasa nchini humo ulioibua malalamiko na upinzani wa vyama na mirengo mbalimbali ya kisiasa khususan chama cha Kiislamu cha An Nahadhah.  

Wapinzani wa Kais Saeid wanamtuhumu kiongozi huyo kuwa amefanya mapinduzi dhidi ya mafanikio ya kidemokrasia yaliyopatikana katika vuguvugu la mapambano ya mwaka 2011 yaliyomuondoa madarakani dikteta Zainul Abidin bin Ali;  hata hivyo yeye mwenyewe anasema, hatua alizochukua ni halali na kwamba kulikuwa na udharura wa kufanya hivyo ili kuiokoa Tunisia na kuzama kwenye dimbwi la mgogoro wa kisiasa wa muda mrefu.../ 

Tags