Jul 02, 2022 02:23 UTC
  • Jeshi la Nigeria laua wabeba silaha 82 jimboni Zamfara

Jeshi la Nigeria limetangaza habari ya kuangamiza makumi ya wanachama wa genge moja la wabeba silaha katika jimbo la Zamfara, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Wizara ya Ulinzi ya Nigeria imesema jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kuua wanachama 82 wa genge hilo katika operesheni ya mashambulizi ya anga iliyopewa jina la "Hadin Kai”.

Taarifa ya wizara hiyo imeeleza kuwa, mbali na wabeba silaha 82 kuangamizwa, wengine wengi wametoroka wakiwa na majeraha katika eneo la Bakura.

Taarifa hiyo haijaeleza iwapo genge hilo lililoshambuliwa ni la kigaidi au ni moja ya magenge ya kijambazi yanayofanya jinai nyinginezo katika jamii. Wizara ya Ulinzi ya Nigeria imeongeza kuwa, wahalifu hao waliokuwa wamejizatiti kwa silaha waliuawa katika operesheni iliyofanyika Alkhamisi.

Jeshi la Nigeria likishika doria katika jimbo la Zamfara

Licha ya kwamba jeshi la Nigeria lilipiga kambi katika jimbo hilo la kaskazini magharibi mwaka 2016 kwa ajili ya kuimarisha usalama, lakini bado makundi ya wabeba silaha ambayo yamekuwa yakifanya wizi na magendo, yanaendelea kufanya jinai na uhalifu.

Mapema mwaka huu, wanavijiji 200 waliuawa katika mashambulizi ya makundi hayo ya wabeba silaha katika jimbo hilo la Zamfara la kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Tags