Jul 02, 2022 11:47 UTC
  • Waandamanaji wenye hasira wavamia jengo la bunge la Libya mjini Tobruk

Waandamanaji waliokuwa na hasira wamevamia jengo la bunge katika mji wa Tobruk mashariki ya Libya wakilalamikia hali duni ya maisha na mkwamo wa kisiasa unaoendelea nchini humo.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, waandamanaji hao, wengi wao wakiwa ni vijana waliokuwa na hasira walifanikiwa kupenya hadi ndani ya jengo la bunge jana Ijumaa na kufanya vitendo kadhaa vya uharibifu, sambamba na kuchoma moto matairi ya magari.

Baadhi ya duru za habari zimeripotiwa kuwa jengo la bunge lenyewe, ambalo katika siku ya mapumziko ya mwisho wa wiki lilikuwa tupu, lilichomwa moto pia.

Waandamanaji hao walipaza sauti wakisema: "Tunataka taa tufanye kazi".

Mapema jana hiyohiyo yalifanyika maandamano pia katika miji mingine kadhaa ya Libya. Katika mji mkuu Tripoli magharibi mwa nchi, mamia ya watu walikusanyika katika mzunguko mkuu na kutoa nara na kulimbiu dhidi ya wanamgambo wanaobeba silaha sambamba na kudai ugavi bora wa umeme na kupunguzwa bei za mikate.

Abdul Hamid Dbaibah (kushoto) na Fathi Bashagha

Taswira zilizosambazwa na vyombo vya habari za maandamano ya upinzani yaliyofanyika Tobruk zimeonyesha mtu mmoja akiendesha buldoza ambalo liliponda sehemu ya lango la kuingilia jengo la bunge na kuwawezesha waandamanaji wengine kuingia bungeni humo kiurahisi. 

Tovuti ya habari ya al-Wasat imeripoti kuwa waandamanaji katika mji wa Tobruk wametaka bunge livunjwe ili ufanyike uchaguzi mpya. Aidha, wamelalamikia hali duni ya maisha waliyonayo raia.

Kwa sasa, kuna serikali mbili zinazovutana juu ya kuhodhi madaraka ya nchi huko Libya.

Katika mji mkuu Tripoli uongozi wa nchi uko mikononi mwa waziri mkuu wa mpito Abdul Hamid Dbeibah. Nayo serikali iliyoundwa na aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani Fathi Bashagha baada ya kuchaguliwa na bunge lenye makao yake Tobruk, inadai ustahiki wa kuongoza nchi.../

Tags