Jul 03, 2022 04:11 UTC
  • Nchi za Afrika Magharibi zajadili vikwazo vya baada ya mapinduzi ya kijeshi

Viongozi wa Afrika Magharibi wanakutana leo Jumapili kutathmini mustakabali wa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya nchi tatu ambako jeshi limechukua mamlaka.

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) imeweka vikwazo vikali vya kiuchumi na kifedha dhidi ya Mali na adhabu ndogo kwa Burkina Faso na Guinea baada ya wanajeshi kuchukua madaraka katika nchi hizo.

Katika mkutano wa kilele wa siku moja katika mji mkuu wa Ghana Accra, ECOWAS itaamua kama hatua hizi zinapaswa kudumishwa, kuimarishwa au kuondolewa.

Ajenda kuu katika mazungumzo yao leo ni  matakwa ya ECOWAS kwamba tawala za kijeshi ziweke ratiba ya mapema ya kurejesha utawala wa kiraia.

Mali, nchi maskini na isiyo na bahari iliyo katika mzozo wa muongo mmoja wa magaidi wakufurishaji imekuwa chini ya vikwazo vya kibiashara na kifedha tangu Januari, hatua ambayo imedhoofisha uchumi wake.

Kikao cha ECOWAS baada ya mapinduzi ya kijeshi Burkina Faso

Burkina Faso, nchi nyingine ya Sahel iliyokumbwa na machafuko ya magaidi wakufurishaji na Guinea hadi sasa zimesimamishiwa uanachama wa bodi za ECOWAS ambayo ina jumla ya wanachama 15.

Nchi hizo tatu zilipitia mapinduzi manne katika kipindi cha miezi 18; mawili nchini Mali mwezi Agosti 2020 na Mei 2021, moja nchini Guinea Septemba 2021 na moja nchini Burkina Faso Januari mwaka huu.

ECOWAS inahofia kuwa homa ya mapinduzi ya kijeshi inaweza kuenea katika nchi zingine na hivyo inawashinikiza  watawala wa kijeshi kuharakisha kurejea kwa uongozi wa kiraia.

Mnamo Juni 4, umoja huo ulikwepa kutoa uamuzi wa vikwazo na badala yake ukajipa mwezi mwingine wa kufanya mazungumzo.