Jul 03, 2022 04:14 UTC
  • Magaidi wa Al-Shabaab waua wanajeshi 5 wa Umoja wa Afrika nchini Somalia

Takriban wanajeshi watano waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mlipuko wa barabarani uliolenga vikosi vya Umoja wa Afrika nchini Somalia siku ya Jumamosi.

Msafara wa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) uligonga bomu la kutegwa ardhini kwenye viunga vya Marka, mji mkuu wa mkoa wa kusini magharibi mwa eneo la Lower Shabelle.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani, Wanajeshi watano waliouawa walikuwa ni wa Uganda na walikuwa wakihudumu katika kikosi hicho cha Umoja wa Afrika

Kundi la kigaidi la al-Shabaab limedai kuhusika na shambulio hilo.

Umoja wa Mataifa umekuwa ukifadhili askari wa Umoja wa Afrika wapatao 21,000, ambao wamekuweko nchini Somalia tokea mwaka 2007. Wanajeshi wa AMISOM ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone, huku maafisa wa polisi wa kikosi hicho cha AU wakitoka Nigeria, Sierra Leone na Uganda.

Mwezi Aprili  Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipangua Kikosi cha Kijeshi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) na kuunda kikosi kipya cha amani cha mpito cha ATMIS. Kikosi hicho cha mpito cha Umoja wa Afrika (ATMIS) kinatazamiwa kumaliza shughuli zake mwaka 2024.

Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 na katika miaka ya hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia kushadidi hujuma za magaidi wakufurishaji wa Al Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo matatizo makubwa. Ingawa kikosi cha Umoja wa Afrika kimefanikiwa kuangamiza idadi kubwa ya magaidi wa Al Shabab lakini bado wanaendelea kutekeleza mashambulizi ya kuvizia mara kwa mara na pia wanaendelea kushikilia baadhi ya maeneo ya Somalia.