Jul 03, 2022 07:40 UTC
  • Wafanyakazi Tunisia wasema Katiba mpya inatishia demokrasia

Muungano mkubwa zaidi wa wafanyakazi nchini Tunisia UGTT umepinga vikali azma ya Rais Kais Saeid wa nchi hiyo ya kuifanyia mabadiliko katiba ya nchi kwa maslahi yake binafsi, ukisisitiza kuwa mpango huo ni tishio kubwa kwa demokrasia nchini humo.

Katika taarifa jana Jumamosi, muungano huo umeeleza bayana kuwa, rasimu ya katiba mpya ya nchi hiyo inayonuia kumuongeza nguvu na mamlaka rais wa nchi ni tishio kubwa kwa demokrasia ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Wiki iliyopita, Rais Kais Saeid wa Tunisia alizindua rasimu hiyo ya katiba mpya ambayo ndani yake inashuhudiwa kwa uwazi jinsi rais huyo alivyoongezewa mamlaka ya utawala. Rasimu ya katiba mpya ya Tunisia imepangwa kupigiwa kura ya maoni tarehe 22 ya mwezi huu wa Julai.

Mnamo Juni 25 mwaka jana, Rais Kais Saeid alihodhi madaraka ya nchi kwa kutekeleza hatua kadhaa za aina yake ikiwemo kulisimamisha Bunge na kumfuta kazi spika wake, pamoja na waziri mkuu wa serikali, na kuchukua udhibiti wa mambo yote ya nchi.

Rais Kais Saeid wa Tunisia

Hatua ya Rais Saed ya kuifuta kazi serikali ilisababisha mkwamo mkubwa wa kisiasa nchini humo ulioibua malalamiko na upinzani wa vyama na mirengo mbalimbali ya kisiasa khususan chama cha Kiislamu cha An Nahadhah.  

Wapinzani wa Kais Saeid wanamtuhumu kiongozi huyo kuwa amefanya mapinduzi dhidi ya mafanikio ya kidemokrasia yaliyopatikana katika vuguvugu la mapambano ya mwaka 2011 yaliyomuondoa madarakani dikteta Zainul Abidin bin Ali.

Tags