Jul 03, 2022 07:49 UTC
  • Kasisi akamatwa Nigeria kwa 'kuwashika mateka' kanisani watu 77

Watu karibu 80 waliokuwa wameshikwa mateka na kasisi mmoja ndani ya kanisa huko nchini Nigeria, wameokolewa katika operesheni ya maafisa usalama.

Duru za habari zimeripoti kuwa, mchungaji huyo aliyewashika mateka watu 77 wakiwemo watoto wadogo 23 huko kusini magharibi mwa nchi amekamatwa. Aidha naibu wake, Josiah Peter Asumosa ametiwa mbaroni.

Habari zaidi zinaarifu kuwa, kasisi huyo anayeitwa David Anifowoshe wa Kanisa la Kipentekosti, aliwaweka mateka watu hao katika orofa ya chini ya jengo la kanisa hilo katika wilaya ya Valentino, jimboni Ondo, kusini magharibi mwa Nigeria.

Afisa wa Mawasiliano na Uhusiano Mwema wa Jeshi la Polisi katika jimbo la Ondo, Funmilayo Odunlami, amesema kiongozi huyo wa Kikristo yuko kizuizini, na kwamba uchunguzi juu ya utekaji huo unaendelea.

Inaarifiwa kuwa, baadhi ya wafuasi wa kasisi huyo walikuwa wamefungiwa kwenye kanisa hilo kwa miezi kadhaa, eti wakisubiri ujio wa pili wa Nabii Isa Masih AS, uliotazamiwa kufanyika tangu mwezi Aprili mwaka huu.

Katika miaka ya hivi karibuni, makundi yenye silaha na magenge ya wahalifu nchini Nigeria yamekuwa yakishambulia vijiji na kuua watu ovyo, na wakati mwingine wanavijiji wamekuwa wakichukuliwa mateka kwa shabaha ya kutumiwa kwa ajili ya kuitisha vikomboleo.

Tags