Jul 04, 2022 04:11 UTC
  • Mwisho wa uwepo wa wanajeshi wa Ufaransa nchini Mali

Sambamba na kuendelea kwa mvutano kati ya Ufaransa na Mali, hatimaye Paris imetangaza ukomo wa kuwepo kwa vikosi vya askari wa nchi za Ulaya vinavyojulikana kama Takuba, nchini Mali. Vikosi vya jeshi la Ufaransa vimekuwepo nchini Mali kwa takriban miaka 10 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.

Mvutano kati ya Ufaransa na Mali ulipamba moto katika miezi ya hivi karibu baada ya mapinduzi ya kijeshi ya 2021 katika nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika, wakati Kanali Assimi Goïta alipotwaa madaraka ya nchi. Maafisa wa serikali ya Mali wanawatuhumu wanajeshi wa Ufaransa kuwa wanashirikiana na makundi ya kigaidi yanayotaka kujitenga eneo la kaskazini mwa nchi hiyo, kufanya ukatili dhidi ya raia na kushindwa kukabiliana ipasavyo na makundi ya kigaidi. Baada ya Baraza la Kijeshi la Mali kuanza kazi lilitangaza kuwa haliyatambui makubaliano ya ulinzi baina ya nchi hiyo na Ufaransa na kwamba halitayatekeleza. Serikali ya Mali pia ilimfukuza balozi wa Ufaransa mjini Bamako, kitendo ambacho kilikabiliwa na hisia kali ya Ufaransa.

Kanali Assimi Goïta

Ufaransa imekuwa ikiendesha shughuli zake katika nchi za Afrika eneo la Sahel, ikiwemo Mali, kwa miaka mingi kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kuimarisha amani. Takriban wanajeshi 4,500 wa Ufaransa wamekuwa katika eneo hilo katika fremu ya "Operesheni Barkhane", kwa madai ya kuzisaidia nchi za eneo hilo; hata hivyo nyaraka zilizochapishwa zinaonyesha kuwa wanajeshi hao wa Ufaransa hawakufanikiwa katika operesheni za kupambana na ugaidi, na hata wakati mwingine wamekuwa wakiwalenga raia wa kawaida. 

Kituo cha Utafiti wa Kistratijia Barani Afrika kimetangaza katika ripoti yake kwamba, matukio ya vurugu na ghasia za makundi ya kigaidi yameongezeka kwa asilimia 70 katika nchi za Sahel na hali hiyo imeweka rekodi mpya ya visa vya ukatili barani Afrika mwaka 2021.

Hali ya kisiasa na kiusalama katika eneo la Sahel hususan nchini Mali inaonesha kuwa, Ufaransa imekuwa ikijaribu kuendeleza siasa zake za kikoloni kwa sura mpya ya ukoloni mamboleo badala ya kupambana na magaidi katika eneo hilo. Ni kwa sababu hiyo ndipo Waziri Mkuu wa Mali, Choguel Kokalla Maïga akasema: Serikali ya sasa imejifunza kutokana na matukio ya dunia katika miaka ishirini au thelathini iliyopita na inajua kwamba Paris bado inataka kufufua satua na ubeberu wake barani Afrika.

Choguel Kokalla Maïga

Kutokana na misimamo hiyo ya viongozi wa Bamako, Ufaransa imetangaza kuwa itawaondoa wanajeshi wake katika ardhi ya Mali. Hata hivyo Paris imesema askari hao watahamishiwa katika nchi nyingine za Sahel Afrika. Hii inaonesha kuwa, Ufaransa haiko tayari kuondoka katika eneo hilo, hasa kwa kutilia maanani utajiri mkubwa wa nchi hizo za Afrika katika sekta ya madini ya urani yanayohitajiwa sana na Ufaransa.

Ukweli ni kwamba nchi nyingi za Afrika hazitaki kupokea majeshi ya nchi za kigeni katika ardhi zao. Kielelezo cha ukweli huo ni maandamano ya wananchi katika miji mikuu kadhaa ya nchi za Afrika ambapo raia walikuwa wakipiga nara zinazopinga ukoloni mamboleo wa ufaransa. Waandamanaji hao waliharibu vituo kahaa vya mafuta ya petroli vya kampuni ya Total ambayo ni nembo ya Ufaransa.

Wamali wakiandamana dhidi ya Ufaransa.

Louis Magloire Komayou, mtaalamu wa wa masuala ya Afrika asema: "Watu wa Mali wanawatazama wanajeshi wa Ufaransa kama jeshi vamizi na linaloikalia kwa mabavu ardhi ya nchi yao."

Hata hivyo, ni jambo lililombali kwamba Wafaransa wataacha udhibiti wao huko Mali na katika nchi nyingine za Sahel. Kwa sababu hiyo inatabiriwa kwamba, vikosi vya jeshi la Ufaransa vitapelekwa Niger au Chad baada ya kuondoka Mali.

Tags