Jul 04, 2022 07:12 UTC
  • Zambia kujenga bomba la dizeli kutoka Tanzania

Zambia imeanza kujenga bomba lenye urefu wa kilomita 700 (maili 435) ili kuingiza mafuta ya dizeli kutoka nchi jirani ya Tanzania ambapo uwekezaji wa awali wa mradi huo ni dola milioni 300.

Waziri wa Nishati wa Zambia Peter Kapala alisema Jumapili kwamba bomba hilo jipya litaenda sambamba na la sasa lakini litakuwa la kisasa zaidi.

Kapala amefafanua zaidi kwa kusema, "Baada ya miezi michache, bomba litaanza kusukuma mafuta ya dizeli nchini Zambia. Awamu ya kwanza ya bomba itaishia Mpika (Wilaya ya Kaskazini mwa Zambia), awamu ya pili Ndola (Mkoa wa Copperbelt) na awamu ya tatu Solwezi (kaskazini magharibi mwa Zambia),"

Hata hivyo, hakutoa maelezo yoyote kwa awamu ya pili na ya tatu ya mradi huo.

Zambia na Tanzania tayari zinatumia Bomba la Tazama, bomba lenye urefu wa kilomita 1,710 (maili 1,063) linalosafirisha mafuta ghafi ya petroli kutoka bandari ya Dar es Salaam nchini Tanzania hadi Kiwanda cha Kusafisha Petroli cha Indeni huko Ndola, Zambia.

Bomba hilo, hata hivyo, limepata uchakavu kutokana na vifaa vyake kuchakaa.

Nchi hizo mbili zilitangaza mnamo 2019 mipango ya kujenga bomba la dola bilioni 1.5 ili kuimarisha usafirishaji mafuta ghafi ya petroli.

Serikali mpya ya Zambia ambayo iliingia ofisini miezi 10 iliyopita imeanza mazungumzo kuhusu mradi huo.

Kapala alisema bomba la dizeli, ambalo litakuwa na ubora wa hali ya juu zaidi kuliko Tazama, litakuwa muhimu katika malengo ya muda mrefu ya nchi ya kuleta utulivu wa usambazaji wa dizeli na kudumisha bei nzuri ya reja reja.

Matumizi ya sasa ya dizeli ya kila siku nchini Zambia yanakaribia lita milioni mbili, huku watumiaji wakuu wakiwa migodini, na kiwango cha usambazaji wa bidhaa nchini humo kimesalia kuwa shwari licha ya changamoto za vita nchini Ukraine.

Taifa hilo la kusini mwa Afrika hata hivyo halijaepushwa na athari za bei ya juu ya mafuta duniani huku lita moja ya dizeli kwenye soko la ndani ikiuzwa kwa takribani dola 2.