Jul 04, 2022 10:58 UTC
  • Ripoti: Nusu ya watu wa Somalia wanahitaji msaada wa haraka wa chakula

Maeneo ya kandokando ya mji mkuu wa Somalia, Mogadishu yamekumbwa na wimbi kubwa la wakimbizi wanaolazimika kukimbia makazi yao kutokana na njaa iliyosababishwa na ukame mkubwa huko kusini na magharibi mwa Somalia.

Mamia ya wakimbizi hao wameonekana wakisubiri misaada ya chakula ya wahisani katika safu ndefu huku wengi wao wakionekana kuchoka na katika hali ya kusikitisha kutokana na umaskini na mashaka ya njaa.

Wakimbizi hao wanaoishi katika vibanda visivyo na mahema ya kuweza kuwakinga na jua au baridi, wamekimbia maeneo yao kutokana na ukame ulioangamiza mimea na mifugo yao na wanaonekana kutelekezwa na mashirika ya misaada ya ndani ya nje ya Somalia.

Baadhi ya wakimbizi hao wanasema kuwa, wanaishi kwa kutegemea misaada ya pale na pale ya wahisani ya chakula kinachokusanywa na raia wa Mogadishu.

Kulingana na ripoti iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Somalia Juni 25, ukame umeathiri Wasomali milioni 7, ambao wanaunda zaidi ya asilimia 42 ya wakazi milioni 15 wa nchi hiyo, na umewalazimisha wanavijiji 684,000 kuhama maeneo yao.

Somalia

Awali ripoti ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ilionyesha kuwa watoto milioni 1.5 wa Somalia wanakabiliwa na utapiamlo kutokana na hali ya ukame, 356,000 kati yao watakabiliwa na hatari ya kifo kutokana na utapiamlo mkali kabla ya mwisho wa mwezi Septemba mwaka huu.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, takriban nusu ya watu wa Somalia (watu milioni 7.7) wanahitaji msaada wa chakula, na kwamba wengi wao wameathiriwa na ukame.

Ofisi hiyo imesema, madhara ya mzozo wa sasa wa Ukraine kwenye usambazaji wa chakula yamezifanya familia za Kisomali kushindwa kumudu kasi ya kupanda kwa bei ya vyakula, huku chakula cha ndani kikipungua. Bei ya vyakula vinavyoagizwa kutoka nje nchini Somalia imepanda kwa asilimia 160 na kuziacha familia za kipato cha chini katika njaa na ufukara.

Tags