Jul 04, 2022 14:08 UTC
  • Watu wasiopungua 27 wauawa katika hujuma mbili za kigaidi, Burkina Faso

Watu wanaoshukiwa kuwa wanachama wa makundi ya kigaidi ya al Qaida na Daesh wameuwa watu wasiopungua 27 katika mashambulizi mawili dhidi ya vijiji vya kaskazini mwa Burkina Faso.

Afisa usalama wa serikali ya nchi hiyo amesema, takriban watu 15, baadhi yao wakiwa watoto, waliuawa Jumapili usiku huko Bourasso katika mkoa wa Kossi, kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.

Afisa huyo amesema: “Watu waliokuwa na silaha walizunguka kijiji na kuanza kuwafyatua watu risasi usiku wa kuamkia leo Jumatatu . 

Watu wengine watu 12 waliuawa siku ya Jumamosi kaskazini mwa Burkina Faso, katika shambulio lililofanyika huko Namissiguima katika jimbo la Yatenga.

Burkina Faso ni miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani na imekuwa ikikabiliana na waasi wa makundi ya kigaidi ya Daesh na al Qaida waliotokea nchi jirani ya Mali mwaka 2015.

Mashambulizi ya waasi hao yamegharimu maisha ya maelfu ya watu na kuwalazimisha takriban watu milioni 1.9 kuyakimbia makazi yao.

Takwimu zinaonesha kuwa, zaidi ya asilimia 40 ya ardhi ya Burkina Faso iko nje ya udhibiti wa serikali. 

Mwezi Januari mwaka huu Burkina Faso ilikumbwa na mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani rais mteule, Roch Marc Christian Kabore.

Kiongozi wa sasa wa nchi hiyo, Luteni-Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba, alitangaza usalama kuwa kipaumbele chake cha kwanza lakini baada ya utulivu wa muda, mashambulizi yalianza tena nchini Burkina Faso na kusababisha mauaji ya mamia ya watu.