Jul 05, 2022 01:01 UTC
  • Misri kuanza mazungumzo ya kitaifa leo Jumanne bila ya Ikhwanul Muslimin

Bodi mpya ya wadhamini yenye wanachama 19 iliyoundwa kwa ajili ya mazungumzo ya kitaifa ya Misri itakuwa na mkutano wake wa kwanza leo Jumanne; ikiwa ni ishara ya kuashiria kuanza mazungumzo kati ya vyama vya siasa yaliyoitishwa na Rais wa nchi hiyo, Abdel Fattah al Sisi, mwezi Aprili mwaka huu.

Mazungumzo hayo ya kitaifa ya Misri yamepangwa kufanyika saa saba mchana kleo Jumanne katika makao makuu ya Akademia ya Mafunzo ya Taifa (NTA). Haya yameelezwa na Diaa Rashwan, Mratibu Mkuu wa mazungumzo hayo na mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Misri.  

Katika mkutano huo wa awali, bodi hiyo mpya ya wadhamini kwa ajili ya mazungumzo ya kitaifa ya Misri itachunguza ratiba ya vikao vya mazungumo hayo sambamba na kuchukua maamuzi na kuweka wazi mijadala ili kupata maoni ya wananchi.

Rashwan amesema lengo la mazungumzo hayo ni kuhakikisha kuwa wananchi wanashirikishwa kupitia njia kadhaa za moja kwa moja na zile za kielektroniki. Ameongeza kuwa, baada ya mikutano ya Bodi ya Wadhamini, kutakuwa pia na kikao cha waandishi wa habari wa ndani na nje nchi ili kuhakikisha kunakuwepo uwazi katika mchakato wa mazungumzo, na wananchi wanapatiwa taarifa haraka kuhusu yaliyozungumzwa vikaoni. 

Akizungumza wiki iliyopita, Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri alieleza kuwa, serikali imeanzisha mazungumzo ya kitaifa kati ya wasomi, vyama na makundi yote ya kisiasa na kuongeza kuwa, ni kundi moja tu ambalo limeondolewa katika mazungumzo hayo akimaanisha Harakati ya Ikwwanul Muslimin iliyopigwa marufuku. 

Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri 

Al Sisi alidai kuwa, Ikhwanul Muslimin ilikataa pendekezo alilolitoa Julai mwaka 2013 la kuitisha uchaguzi wa mapema huko Misri ili kutatua mgogoro nchini humo baada ya wananchi kuandamana dhidi ya kundi hilo na badala yake Ikhwanul Muslimin iliamua kuchochea mapigano. 

Harakati ya Kiislamu ya Ikwanul Muslimin ndio chama na kundi kubwa zaidi la kisiasa nchini Misri. 

Tags