Jul 05, 2022 01:01 UTC
  • Kamati ya Katiba Tunisia yapinga rasimu ya katiba iliyopendekezwa na Rais

Mkuu wa Kamati ya Katiba ya Tunisia ametangaza upinnzani wake dhidi ya rasimu ya katiba mpya iliyotangazwa na Rais Kais Saeid wa nchi hiyo, akisema kuwa Rais Saeid anapigania kuwepo katiba ya upande mmoja nchini humo.

Sadok Belaid ambaye ni profesa wa zamani katika masuala ya sheria na katiba amesema kuwa, rasimu iliyozinduliwa na Rais wa Tunisia ni hatari na haiendi sambamba na rasimu ya awali iliyotayarishwa na kamati hiyo. Amesema, ni jukumu lao kupinga kwa nguvu suala hilo na kwamba, rasimu hiyo iliyozinduliwa na Rais Kais Saeid haina mlingano na haifanani na ile waliyoitayarisha na kuituma kwake. Profesa Belaid amesema, rasimu hiyo ina sura ambazo zinaweza kufungua ukurasa wa kuundwa utawala wa kidikteta nchini Tunisia.

Mwaka jana, Rais wa Tunisia aliifuta kazi serikali na kutwaa madaraka ya utendaji ya nchi na hivyo kuasisi utawala wa mtu mmoja. Hadi sasa Rais wa Tunisia hajasema lolote kuhusu katiba tangu achapishe rasimu hiyo ya katiba aliyoipendekeza Alhamisi iliyopita katika gazeti rasmi la serikali. 

Tunisia inatarajia kuitisha kura ya maoni kuhusu katiba mpya tarehe 25 mwezi huu wa Julai. Kwa mujibu wa rasimu iliyopendekezwa na Rais Saeid kwa ajili ya katiba mpya, Rais Saeid ataruhusiwa kuwasilisha miswada ya sheria na kuwa na mamlaka makubwa ya kupendekeza mikataba mbalimbali na kuandaa bajeti za serikali.  

Katika siku za karibuni, Watunisia wamemimika katika mitaa na barabara za nchi hiyo wakipinga rasimu ya katiba iliyopendekezwa na Rais wao. 

Watunisia wapinga rasimu ya katiba mpya 

 

Tags