Jul 06, 2022 06:26 UTC
  • UN yagundua makaburi mengine ya umati nchini Libya

Jopo la Umoja wa Mataifa nchini Libya limetangaza habari ya kugundua 'makaburi ya umati' ambayo hayajafanyiwa uchunguzi, huku likiitaka Tripoli ifanye upekuzi zaidi na kuyachunguza makaburi yaliyogunduliwa.

Jopo hilo linatazamiwa wiki hii kulikabidhi Baraza la Haki za Binadamu la UN ripoti kuhusu makaburi hayo mapya ya umati yaliyogunduliwa katika mji wa Tarhauna, magharibi mwa Libya. Jopo hilo la Umoja wa Mataifa nchini Libya limebainisha kuwa, yumkini makaburi hayo ya umati yanapindukia 100.  

Limeeleza namna genge la wanamgambo lililokuwa likiongozwa na ndugu saba liliua na kuwazuilia mamia ya watu kati ya mwaka  2016-2020 katika mji huo.

Jopo hilo la UN limesema genge hilo lilikuwa likiwatesa na kuwakandamiza watu waliokuwa wakishikiliwa na kundi hilo katika jela zao, baadhi wakiwekwa kwenye kijisanduku kinachofanana na tanuri, na kisha kuwachoma moto wakati wa kuwasaili.

Mji wa Tarhauna ulioko yapata kilomita 90 kusini mwa mji mkuu Tripoli, ulikuwa ngome ya vikosi vya Jenerali muasi Khalifa Haftar wakati wa kampeni zao za kutaka kuiteka Tripoli, mji mkuu wa Libya.

Libya imeathiriwa na machafuko na uksoefu wa amani tangu kupinduliwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011 kwa uingliaji wa nchi ajinabi. 

Tags