Jul 06, 2022 13:39 UTC
  • Katibu Mkuu wa OPEC, Barkindo, afariki dunia

Mohammed Sanusi Barkindo, katibu mkuu wa Shirika la Nchi Zinazozalisha Mafuta ya Petroli Kwa Wingi Duniani OPEC ameaga dunia, mkuu wa shirika la mafuta la serikali ya Nigeria ametangaza leo Jumatano.

Mele Kyari, Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Petroli la Nigeria, ameandika katika ujumbe wa Twitter kwamba Barkindo aliaga dunia mwendo wa saa 11 jioni kwa saa za huko Jumanne. Hakueleza sababu ya kifo.

Kwa mujibu wa gazeti la Business Day la Nigeria, Barkindo alikuwa nchini kwake, Nigeria. Alikutana na Rais Muhammadu Buhari siku ya Jumatatu, na baadaye akatoa hotuba katika mkutano wa mafuta na gesi siku ya Jumanne, gazeti hilo limesema.

Katika kikao hicho Buhari alimtaja Barkindo kuwa balozi mzuri wa nchi yake. Barkindo aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa OPEC mnamo 2016 na muhula wake ulikuwa unamalizika mwezi huu wa Julai. OPEC tayari ilikuwa imemchagua Haitham al-Ghais kuwa katibu mkuu mpya wa shirika hilo.

OPEC ina mataifa 13 yanayozalisha mafuta ya petroli kwa wingi duniani kutoka Mashariki ya Kati, Afrika na Amerika Kusini, zikiwemo Saudi Arabia, Iran, Iraq, UAE, Nigeria na Venezuela. Wauzaji nje wengine wakuu, kama vile Russia, wana hadhi ya waangalizi katika kundi hilo.