Jul 06, 2022 13:45 UTC
  • Msafara wa Rais wa Nigeria washambuliwa, watu kadhaa wauawa

Watu kadhaa wameuawa, huku wengine wakijeruhiwa Jumanne, wakati majambazi waliposhambulia msafara wa walinzi, maafisa wa itifaki na vyombo vya habari, kabla ya safari ya Rais Muhammadu Buhari kufika katika mji alikozaliwa wa Daura, Jimbo la Katsina.

Ofisi ya Rais wa Nigeria imetoa taarifa na kuitaja hujuma hiyo ya Jumanne kuwa ni ya kusikitisha.

Katika taarifa iliyotolewa Jumanne usiku na msemaji wa rais, Mallam Garba Shehu, ofisi ya rais amedokeza kuwa watu wachache walifariki, huku watu wawili, waliopata majeraha wakati wa shambulio hilo tayari wakipokea matibabu.

Amesema wafanyakazi na maafisa wengine katika msafara huo walifika salama mjini Daura. Msafara huo ulikuwa unatangulia kabla ya ule wa asili wa Rais Buhari kufika eneo hilo.

Taarifa iliyokuwa na kichwa cha maneneo kisemacho,  "Walinzi Shujaa wa Rais Wazuia Mashambulizi Dhidi ya Timu ya Utangulizi ya Ziara ya Rais", imesema kuwa, tukio la ufyatulianaji risasi lilitokea karibu na Dutsinma, Jimbo la Katsina kaskazini mashariki mwa Nigeria.

"Washambuliaji walifyatua risasi kwenye msafara huo kutoka maeneo ya kuvizia lakini walizuiwa na wanajeshi, polisi na maafisa wa kikosi cha DSS walioandamana na msafara huo.

"Watu wawili katika msafara huo wanapokea matibabu kutokana na majeraha madogo waliyoyapata na wafanyakazi wachache waliopoteza maisha wamelazwa hospitalini. Wafanyakazi wengine wote, na maafisa pamoja na magari yao walifika salama hadi Daura," taarifa hiyo imesema.

Buhari amepangiwa kuzuru Katsina wakati wa sherehe ya Sallah, tamasha la Kiislamu la Sala ya Idul Adha, ambalo litafanyika mwishoni mwa juma.