Jul 06, 2022 13:52 UTC
  • Bei ya mafuta ya petroli nchini Tanzania yapanda licha ya ruzuku

Watanzania wanakabiliana na nyakati ngumu kutokana na bei ya mafuta kupanda nchini kote kuanzia leo Jumatano, licha ya ruzuku ya serikali.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), bei za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa zimepanda hadi kiwango ambacho hakijawahi kurekodiwa katika soko la ndani.

Kuanzia Julai 6, 2022, lita moja ya petroli sasa inagharimu Tsh3,220 ($1.38) jijini Dar es Salaam kutoka Tsh2,994 ($1.28) mwezi uliopita, wakati ile ya dizeli sasa itakuwa Tsh3,143 ($1.35) kutoka Tsh3, 131 ($1.34), Ewura imesema katika taarifa.

Kwa mujibu wa Ewura, bei za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa zimepanda hadi kiwango ambacho hakijawahi kurekodiwa katika soko la ndani.

Rais Samia Suluhu wa Tanzania

Bei ya reja reja ya mafuta ya taa itakuwa Tsh3,442 ($1.48) kwa lita kutoka Tsh3,299 ($1.41) mwezi uliopita.

Katika baadhi ya maeneo kama Kagera, lita moja ya petroli inagharimu hadi Tsh3,435 ($1.47).

Hata hivyo, bei zingekuwa za juu zaidi bila ruzuku ya serikali ya mwezi ya Tsh100 (dola milioni 42) iliyoanza Juni.

"Kampuni za uuzaji wa mafuta ziko huru kuuza bidhaa zao kwa bei ambayo inawapa faida ya ushindani mradi bei hiyo haizidi bei kikomo," Ewura imesema katika taarifa iliyosainiwa na mkurugenzi mkuu wake Modestus Lumato.

Mei mwaka huu, Waziri wa Nishati, January Makamba alisema serikali imetoa ruzuku ya Sh100 bilioni kwa ajili ya kupunguza bei ya mafuta nchini, kutolewa kwa ruzuku hiyo hakutagusa miradi ya maendeleo inayoendelea.

“Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kwamba mwaka ujao wa fedha ni mbali. Ahueni itafutwe mapema zaidi. Hivyo basi, kama hatua ya dharura, katika kipindi hiki kabla hatujafikia mwaka mpya wa fedha, serikali ijibane na ijinyime na zitolewe Sh100 bilioni kwa ajili ya kupunguza bei za mafuta hapa nchini."

“Ruzuku hii ya Sh100 bilioni itatolewa kwa ajili ya kupunguza bei ya mafuta kuanzia Juni 1, 2022. Hii ni kutokana na kuwa, wafanyabiashara wa jumla wamekwisha lipia gharama ya mafuta ambayo imejumuishwa katika bei hizi za Mei 2022 na wafanyabiashara wa mafuta katika vituo wamekwishanunua mafuta kwa bei hii inayotumika sasa,” amesema Makamba.