Jul 07, 2022 11:25 UTC
  • DRC na Rwanda zakubaliana kupunguza mivutano kwa sababu ya waasi wa M23

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC na Rwanda zimekubaliana kutekeleza "mchakato wa kupunguza mvutano" baina yao kufuatia mazungumzo ya siku moja yaliyofanywa na marais wa nchi hizo mbili kwa upatanishi wa rais wa Angola.

Hayo yameelezwa na ofisi ya rais Felix Tshisekedi wa DRC, katika ujumbe uliotumwa kwenye mtandao wa Twitter.

Aidha, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda zitafufua kamisheni ya pamoja ya pande mbili, ambayo itaanza tena kazi zake tarehe 12 Julai katika mji mkuu wa Angola, Luanda.

Kufuatia mazungumzo ya marais Felix Tshisekedi wa Kongo DR na Paul Kagame wa Rwanda yaliyofanyika kwa upatanishi wa Rais Joao Lourenco mjini Luanda, pande hizo mbili zimetolewa mwito wa kurejesha katika hali ya kawaida uhusiano wao wa kidiplomasia, kukomesha uhasama uliopo na "kuondoka mara moja na bila masharti yoyote" wanamgambo wa kundi la waasi wa M23 katika maeneo walipo mashariki ya DRC.

Rais Joao Lourenco wa Angola ameteuliwa na Umoja wa Afrika kuwa mpatanishi katika mazungumzo baina ya marais wa DRC na Rwanda.

Wanamgambo wa kundi la M23

Akizungumza mwishoni mwa mazungumzo hayo, Rais Lourenco amesema: "ninafarijika kutangaza kuwa, kwa uoni wetu, tumepata matokeo chanya, ambapo pamoja na mambo mengine, tumekubaliana juu ya usitishaji vita".

Hakuna maelezo yaliyotolewa na serikali ya Rwanda.

Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimekuwa zikishambuliana kwa maneno yaliyochochewa na tuhuma za DRC kwamba serikali ya Kigali inawaunga mkono waasi wa M23 wa nchini Kongo ambao akthari ya wapiganaji wake wanatoka kabila la Tutsi.

Mwezi uliopita, kundi hilo lilikiteka kituo muhimu cha mpakani.

Kwa upande wa Rwanda, nchi hiyo inaituhumu DRC kuwa inaliunga mkono kundi la waasi ambalo baadhi ya wanachama wake walihusika katika mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994.

Kila nchi inazikanusha tuhuma zilizoelekezwa dhidi yake.../

Tags